Jumatatu Simba walishinda 2-0 dhidi ya Ihefu halafu Jumanne watani zao, Yanga wakaibabua Kagera Sugar mabao 5-0, unajua nini kinafuata? Ni Kariakoo Dabi Jumapili hii.
Ikicheza kwa shangwe kubwa mbele ya mashabiki wake pale Dimba la Azam Complex, Yanga juzi ilibeba alama tatu mbele ya Kagera na kuwafanya waendelee kukalia usukani wa ligi kuu wakifikisha pointi 68 kupitia michezo yao 25.
Katika mchezo huo, ilishuhudiwa Aziz Ki akifunga mabao mawili huku moja likiwa la kideoni. Ki aliipa Yanga bao la kwanza kwa penalti dakika ya 43 iliyotokana na Fiston Mayele kufanyiwa madhambi ndani ya 18 kabla ya kufunga kwa shuti kali nje ya 18 dakika ya 45.
Mayele katika dakika 45 za mwanzo alifanya majaribio matano ambayo hayakulenga lango ilikuwa dakika ya 6, 14, 15, 17 na 32 kabla ya kusahihisha makosa dakika ya 50 akimtoka mchezaji wa Kagera kuanzia katikati ya uwanja hadi kuingia ndani ya 18 na kufunga bao lake la 16 kwenye ligi kuu msimu huu.
Baada ya bao hilo, Mayele alipumzishwa na nafasi yake kuchukuliwa na Clement Mzize, sambamba na Bernard Morrison ambaye alichukua nafasi ya Farid Mussa.
Dakika ya 85, mashabiki wakidhani Yanga itaondoka na ushindi huo wa mabao 3-0, Morrison alipiga mkwaju mkali ndani ya 18 na kuandika bao la nne.
Wakati Kagera wanajiuliza niaje ni vipi, Mzize alichomoka na kutaka kwenda kufunga bao la tano lakini aliwahiwa kwa kufanyiwa madhambi ambayo yalizaa penalti iliyopigwa na Aziz Ki ambayo ilizaa hat trick yake ya kwanza tangu ajiunge na wababe hao kutoka Jangwani.
Kagera Sugar chini ya Kocha Mkuu, Mecky Maxime mipango yao kupitia kwa washambuliaji wao ilishindwa kuzaa matunda kutokana na uimara wa safu ya ulinzi ya Yanga iliyokuwa chini ya nahodha Bakari Mwamnyeto.
Kituo kinachofuata sasa ni Dimba la Mkapa Jumapili hii ambapo wakongwe Simba na Yanga watakuwa na kibarua cha kutafuta mbabe kwenye ligi kuu.