Mbilinge za wiki za mashindano ya kimataifa rasmi lilikamilika juzi Jumapili kwa michezo ya Kombe la Shirikisho Afrika kuchezwa kwenye viwanja mbalimbali, sasa timu zinarejea kwenye ratiba ya mashindano ya ndani.
Kwa hapa Tanzania mashindano ya ndani hususani Ligi Kuu Bara yalisimama tangu Machi19, mwaka huu kwa ajili ya kupisha kalenda ya michezo ya kusaka tiketi ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), ambapo Stars walikuwa na kibarua cha kuvaana na Uganda.
Kwenye michezo huyo miwili mtawalia Stars ilishinda mechi moja na kupoteza mchezo mmoja, baada ya hapo wikiendi hii ilichezwa michezo ya mwisho ya hatua ya makundi kimataifa ngazi ya klabu, Simba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Yanga kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
Baada ya ratiba hizo wiki hii vita ya kusaka nusu fainali inaendelea ambapo kuna michezo mikali ya wakubwa ambao watakuwa kazini.
SIMBA VS IHEFU
Kama kuna michezo ambayo inasubiriwa kwa hamu kubwa kwenye hatua hii ya robo fainali basi ni mchezo huu kati ya Simba ambao watakuwa nyumbani kuwavaa Ihefu kutokea mkoani Mbeya.
Kwa nini mchezo huu unasubiriwa kwa hamu? Hii ni kutokana na ubora wa timu zote mbili, lakini zaidi sana kasi na historia ya Ihefu mbele ya timu zenye majina makubwa.
Ikumbukwe Ihefu ndio timu pekee ambayo imefanikiwa kuifunga Yanga kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu, huku pia wakifanikiwa kuifunga Azam, hivyo huenda ukawa mchezo mgumu kwa Simba.
Simba wanaingia katika mchezo huu wakiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wamabao 4-0 dhidi ya African Sports katika hatua ya 16 bora.
Msimu uliopita Simba kwenye mashindano haya waliondolewa kwenye hatua ya nusu fainali na watani zao wa jadi Yanga kwa kipigo cha bao 1-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Kabla ya hapo Simba walikuwa wanatetea ubingwa wa michuano hii kwa misimu miwili mfululizo yaani 2019/20 na 2020/21, hivyo wataingia katika mchezo huu wakiwa na wajibu mmoja mkubwa wa kuhakikisha wanarejesha taji hili ambalo walilipoteza kwa Yanga msimu uliopita.
YANGA VSGEITA GOLD
Baada ya juzi Jumapili kumaliza ratiba ya hatuaya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika walipovaana na TP Mazembe, Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa mashindano haya watashuka uwanjani Jumamosi hii kwenye mchezo wa Robo fainali ya mwisho.
Yanga watavaana na Geita Gold kwenye mchezo ambao unatarajiwa kupigwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Dar es Salaam.
Mchezo huu unatarajiwa kuwa wa kisasi kwa Geita Gold ambao wanakumbuka kipigo cha mabao3-1 kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Machi 12, mwaka huu, kwa Yanga utakuwa mchezo wa kusaka rekodi.
Yanga wamefikia hatua hii baada ya kuwaondosha Tanzania Prisons kwenye hatua ya 16 bora kwa ushindi wa mabao 4-1.