Dini

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Askofu aichongea Halmashauri kwa Rais Samia

Askofu Kwa Samia Askofu aichongea Halmashauri kwa Rais Samia

Tue, 13 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kanisa katoliki Jimbo Kuu la Mwanza limemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kutatua mvutano uliopo kati ya halmashauri ya Wilaya ya Magu na kituo cha hijja cha Kageye ambao umekwamisha baadhi ya shughuli za kanisa hilo ikiwemo ibada.

Ombi hilo limetolewa leo Juni 13, 2023 na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Renatus Nkwande wakati akitoa salamu za kanisa hilo mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye uzinduzi wa tamasha la Bulabo linalofanyika katika uwanja wa Red Cross Ngomeni, Kisesa Wilaya ya Magu, Mwanza.

Askofu Nkwande amesema kituo cha Kageye ni moja ya vituo muhimu vitatu vikiwamo Bukumbi na Malya ambavyo ni sehemu ya historia ya kanisa katoliki Kanda ya Ziwa na vinatumika kwa shughuli za hijja kwa waumini wa kanisa hilo.

Nkwande amesema nia ya kanisa hilo ni kuviunganisha na kuviendeleza vituo vya hija vya Malya, Kageye na Bukumbi kwani ni vituo muhimu na wanataka kuvienzi na kuvitunza ili histori isipotee kwani ndipo matukio mengi ya historia ya ukiristu yalifanyika.

Amesema kwa sasa kituo cha Kageye kina mgogoro ambapo halmashauri ya Wilaya ya Magu inadai ni eneo lake wakati inajulikana ni mali ya kanisa katoliki na ilijengwa na taasisi hivyo, ambapo amemuomba Rais kumaliza mvutano huo.

“Kituo cha Kageye mpaka sasa kuna mvutano na wilaya ya magu wanaodai ni mali yao. viongozi wa halmashauri ya magu wanadai na tunasumbuana nao na siyo lengo letu kuvutana na viongozi wa Serikali,”

“Serikali ilitangaza kituo cha kageye kuwa makumbusho lakini haitunyimi sisi wamiliki kukitumia kituo hicho kwa shughuli zetu za kidini. Tunagombana na kubishana kwa kitu ambacho kiko wazi, kanisa katoliki tulikijenga kwa lengo kwamba watu wakifika pale wafanye ibada zao,”

“Hotuba hii siyo kwamba nalalamika kutokana na hali hii tunaomba uwaruhusu waumini wa dini katika eneo la Kageye waende wakasali katika kigango cha kageye na turuhusiwe tuendelee kutumia kituo cha Kageye kama eneo la hija na makumbusho,” amesema Askofu Nkwande.

Akizungumzia chimbuko la tamasha la kidini na kiutamaduni la Bulabo, Askofu Nkwande amesema lilitokana na nia ya Wamisionari wa Afrika waliofika kueneza neno la mungu mwishoni mwa karne ya 19 ambao walihitaji kueneza neno na kutobadili mila na desturi walizozikuta ama kuwalazimisha waafrika kufuata tamaduni za kizungu ambapo watemi akiwamo Kiganga wa Bukumbi waliwapa maeneo ya kujenga makanisa.

Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla akizungumzia sakata hilo amemhakikishia na kumtoa wasiwasi Askofu Nkwande kuwa uongozi wa mkoa huo utakaa chini na kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa Kageye.

“Suala la Kageye nimelipokea nitalifanyia kazi na tutatoka na ushauri mzuri wa kulijenga kanisa. Mheshimiwa Baba Askofu hili nimelipokea tutalifanyia kazi,” amesema Makalla.

Akifungua tamasha hilo, Rais Samia Suluhu Hassani ameagiza wizara zinazohusika ikiwemo ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kutatua mgogoro huo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: