Wachimbaji wadogo wa madini wanne wakufa kwa kufukiwa na kifusi walipokuwa wakiendelea na shughuli ya kuchimba dhahabu eneo la Mwasabuka Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita.
Ofisa Madini Mkazi Mkoa wa Kimadini wa Mbogwe, Ernest Maganga amesema ajali hiyo ilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita katika eneo la migodi isiyo rasmi.
“Eneo lilikotokea ajali ina leseni ya utafiti na inaamini wachimbaji hawa waliingia na kuanza kuchimba kinyume cha sheria ndipo walipofikiwa na kifusi. Tunashirikiana na vyombo vya dola kuwabaini wanaohusika na vitendo vya kupeleka wachimbaji wadogo katika eneo lile ambalo siyo machimbo rasmi,’’ amesema Maganga
Katibu Tawala Wilaya ya Nyang’hwale, Fabian Sospeter amesema watu watatu walifariki dunia papo hapo wakati mwingine alipoteza maisha wakati akipewa huduma za kitabibu Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Geita alikokimbizwa katika jitihada za kuokoa maisha yake.
Amewataja waliopoteza maisha katika tukio hilo kuwa ni Herry Charles (22), Masalu Charles (35) Manyanda Elias (36) na John Enock (22), wote wakazi wa eneo la Kakola Halmashauri ya Msalala Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.
Wilaya ya Nyang’wale mkoani Geita inapakana na Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga na mara nyingi wakazi wa wilaya hizo mbili huingiliana katika shughuli za kiuchumi na kijamii.
Isack Zenze, mmoja wa wakazi wa Wilaya ya Nyang’wale ameviomba vyombo vya usalama na usimamizi wa masuala ya madini kutimiza wajibu kwa kufuatilia shughuli zote za wachimbaji kuzuia virendo vinavyokiuka sheria ikiwemo uchimbaji holela katika migodi isiyo rasmi.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka mamlaka za madini na Jeshi la Polisi, vifo vya wachimbaji hawa inafikisha idadi ya vifo 13 vya wachimbaji wadogo vilivyoripotiwa mkoani Geita katika kipindi cha Januari, 2023 hadi Aprili, 2023.
Vifo 10 kati hivyo vimeripotiwa kutokea katika maeneo ya migodi isiyo rasmi ambako baadhi ya wachimbaji huvamia na kuchimba madini kinyume cha sheria.