Mfugaji mmoja wa jamii ya Kimaasai aliyefahamika kwa jina la Tumbeine Abdalah mwenye umri wa miaka 45, mkazi wa kijiji cha Mkata Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro ameuawa na tembo usiku wa kuamkia Mei 20, 2023 baada ya kuchomwa na meno ya Tembo nyuma ya mgongo wake pamoja na mguuni kisha meno hayo kutokea upande mwingine.
Baba mdogo wa marehemu aliyefahamika kwa jina la Paul Saiyuki anasema marehemu alivamiwa na Tembo huyo akiwa njiani akirejea nyumbani akiwa na wenzake wanne.
Mwenyekiti wa kijiji cha mkata lilikotokea tukio hilo Samson Magao anasema hili si tukio la kwanza kutokea katika kijiji hicho hivyo wameomba Serikali kuangalia suala hili kwani kijiji chao kipo jirani na hifadhi ya Taifa Mikumi.
Kwa upande wake Afisa Mhifadhi mkuu hifadhi ya Taifa ya Mikumi kitengo cha Ujirani mwema David Kadomo amesema tukio watahakikisha wanaendelea na doria ambazo wanazifanya kila siku ili kudhibiti wanyama hao.
Marehemu ameacha wake wawili na watoto 15 wakiwemo wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari.