Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mke asimulia alivyonusurika kifo, mumewe auawa kwa risasi

Mke Asimulia Mke asimulia alivyonusurika kifo, mumewe auawa kwa risasi

Tue, 23 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ni kudra ya Mwenyezi Mungu! Hiyo ndiyo kauli inayofaa kutumika kuelezea jinsi Mariam Jumanne, mke wa Nixon Gisiri aliyekuwa mfanyabiashara wa madini ya ujenzi katika Kijiji cha Nyankanga Wilaya ya Butiama alivyoepuka kifo wakati watu wanaominika kuwa ni majambazi walipovamia nyumbani kwao na kumuua mume wake kwa kumpiga risasi.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Moses Kaegele, tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Mei 21, 2023 baada ya watu hao waliokuwa na silaha za jadi na za moto kuvamia nyumbani kwa mfanyabiashara huyo kwa kuvunja mlango, kuingia ndani na kushinikiza wapewe Sh15 milioni.

"Tukio la uvamizi lilitokea Saa 8:00 ambapo pamoja na kumpiga risasi mwanaume, watu hao pia walimjeruhi mke wake kwa kumkata panga eneo la kichwani na mdomoni. Mama huyo amelazwa Hospitali ya Wilaya Butiama kwa matibabu,’’ amesema DC Kaegele

Amesema mfanyabiashara Gisiri ambaye sasa ni marehemu alijitahidi kujinusuru kwa kukimbilia kwenye chumba cha watoto baada ya uvamizi, lakini wauaji hao walimfuata huku wakimshinikiza kuwapa Sh15 milioni walizoamini anazo.

Baada ya kutopata fedha, ndipo wauaji hao walipoamua kumpiga risasi ya ubavuni uliosababisha kifo chake, kabla ya kumbaka mmoja wa watoto wa familia hiyo na kutokomea wakichukua seti moja ya runinga na simu ya kiganjani.

 Simulizi ya mke

Akizungumzia tukio hilo, Mariam Jumanne, mke wa marehemu Nixon Gisiri amemshukuru Mungu kwa kuendelea kuwa hai huku akiamini kitendo cha kujifanya amekufa mara baada ya kukatwa panga ndicho kimemnusuru.

‘’Muda mfupi kabla ya uvamizi, tulimsikia mbwa wetu akibweka kwa sauti kuonyesha ishara kwamba ameona watu au kitu cha hatari; hali iliyozua taharuki. Tukiwa tunawaza cha kufanya, ghafla watu walianza kuusukuma mlango wetu kwa nguvu lakini walishindwa kuufungua,’’ amesema Mariam

Amesema baadaye wakahisi watu hao wanatindua ukuta pembeni mwa mlango na ghafla wakaingia ndani huku wakiwamulika kwa tochi yenye mwanga mkali.

‘’Mume wangu alikimbilia chumbani kwa watoto kujificha huku mimi nikiendelea kupiga kelele kuomba msaada kwa majirani, kitendo kilichowakera wavamizi wale na kuamua kunikata kwa panga kichwani na mdomoni,’’ anasimulia mama huyo anayeendelea kuuguza majeraha hospitalini.

Anasema baada ya kuhisi hatari inayomkabili alijiangusha chini na kujifanya amekufa, ndipo wavamizi hao wakamwacha na kumfuata mume wake hadi kwenye chumba cha watoto alikokimbilia wakimshinikiza awape fedha.

‘’Baada ya mume wangu kusisitiza kwamba hakuwa na fedha ndipo wale watu wakampiga risasi na kufariki" anasimulia huku akibubujikwa machozi.

Amesema baada ya kuhisi wazazi wote wamefariki, wavamizi hao wakaanza kuwashinikiza watoto wawaonyeshe sehemu ambako wazazi wao wanatunza fedha; na walipokosa ndipo wakaamua kumuingilia kwa zamu mmoja wa watoto wao kabla ya kuchukua seti ya runinga na simu moja na kutokomea kusikojulikana.

Katika tukio lingine, Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Moses Kaegele amesema usiku huo huo, watu wenye silaha za jadi na za moto waliwavamia vijana 15 wa ulinzi shirikishi vijana 15 wanaojihusisha na ulinzi shirikishi katika Kijiji cha Mmazami na kuwajeruhi kwa kuwakata na vitu vyenye ncha kali.

Amesema tukio la kuvamiwa walinzi shirikishi katika Kijiji cha Mmazami lilitokea Saa 7:00 usiku, muda mfupi kabla ya tukio la uvamizi katika Kijiji jirani cha Nyankanga.

‘’Mmoja wa vijana wa ulinzi shirikishi amepoteza kiganja cha mkono wake,’’ amesema Mkuu huyo wa Wilaya ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama wilaya

Amesema muda mfupi kabla walinzi shirikishi hao waliokuwa wakitimiza wajibu kwa kufanya doria kijijini hawajavamiwa na kuanza kushambuliwa kwa kukatwakatwa, watu wawili waliokuwa wanatumia usafiri wa pikipiki walifika na kujitambulisha kuwa ni askari polisi na kuwaamuru kulala chini.

"Watu hao waliojifanya ni polisi waliwatisha kwa kupiga risasi hewani, na ghafla wakavamiwa na kuanza kukatwakatwa maeneo tofauti ya mwili, hasa vichwani. Tunahisi ni kundi hilo hilo ndilo lilifanya uvamizi kijiji jirani cha Nyankanga. Yawezekana walifanya hivyo kurahisisha uvamizi wao bila kuingiliwa na walinzi wa kijiji jirani cha Mmazami,’’ amesema DC Kaegele

Amesema mlinzi aliyepoteza kiganja cha mkono wake anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mara huku wenzake 14 wakienelea na matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Butiama.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: