Lazaro Nyachuma (66) Mkazi wa Tabata ameuawa kwa kuchomwa kisu na mjukuu wake Nasibu Limba, maarufu Romanus mwenye umri wa miaka 18 usiku wa kuamkia leo, chanzo kikidaiwa kuwa ni ugomvi wa mara kwa mara ndani ya familia.
Mke wa Marehemu ameieleza Azam News kuwa ugomvi uliosababisha kifo hicho baina ya mumewe na mjukuu wake ulianza baada ya babu kutoridhishwa na majibu aliyopewa na mjukuu wake baada ya kumuuliza alipo bibi yake
“Babu alimuuliza bibi yuko wapi, mjukuu akamjibu yupo nje huko, alivyomjibu vile babu akapata jaziba akanyanyuka mzima akamfuata ndani, sasa wakati akimpiga wakaburuzana mpaka sehemu ya pili, pembeni kulikuwa na kabati kina silaha, akachomoa kisu wakaanza kukigombea, nikatoka nje kupiga kelele kuomba msaada, wakati narudi nikakuta babu amechomwa kisu,” amesema mke wa marehemu.
“Mama mwenye nyumba alitoka nje tukamsikia akisema ‘jamani naomba mtusaidie’, tukatoka kuingia ndani tukakuta damu zimejaa.
“Ugomvi ulivyoanza yule babu alisema nitawaua wote, nitaanza na Romanus, atakuja bibi yake nitamalize na huyo mjukuu mdogo pia. Kijana alikuwa akisema mimi nitakuja kutoroka hapa nyumbani sababu ya tabia za babu, ni mkorofi ananyinyanyasa mno,” walisema majirani.
Mzee yule akiwa hajanywa pombe ni mkimya sana, ila akilewa tu anakuwa mkorofi. Mtuhumiwa amesema walikuwa wakitibuana kimaneno mara kwa mara, hasa akolewa. Mtuhumiwa amepatikana na kupelekwa polisi,” alisema mwenyekiti wa mtaa.