Watoto mapacha wenye umri wa mwaka mmoja na miezi sita wamefariki baada ya kutumbukia kwenye dimbwi la maji lililochimbwa nyumbani kwao kwa ajili ya kunyweshea mifugo.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa kwa vyombo vya habari leo Aprili 25, 2023 imewataja watoto waliopoteza maisha katika tukio hilo kuwa ni Kulwa Jimoku na Doto Jimoku, waliokuwa na umri wa mwaka na miezi sita.
Kamanda Mutafungwa amesema watoto hao walifikwa na mauti Saa 8:00 mchana wa Aprili 23, 2023 eneo la Hungumalwa Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza baada ya kutumbukia kwenye dimbwi hilo walipokuwa wakicheza eneo la nyumbani kwao.
"Watoto hawa walikuwa wakicheza michezo ya kitoto umbali wa mita 30 kutoka kwenye nyumba ya wazazi wao wanaijulikana kwa majina ya Jimoku Rozalia (28) na Avelina Nkwaya (20) ndipo walipotumbukia kwenye dimbwi la maji lililochimbwa kwa ajili ya kuhifadhia maji ya kunyweshea mifugo," amesema Mutafungwa
Amesema wakati watoto hao wanacheza jirani na dimbwi hilo, wazazi wao walikuwa wanaendelea na shughuli ya kilimo katika shamba lililopo eneo la nyumbani kwano.
“Jeshi la Polisi linawataka wazazi na walezi kuongeza umakini kwa kufuatilia michezo na eneo wanapocheza watoto wao, hasa kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kunyesha na kusababisha maji kutuama maeneo yenye madimbwi,” amesema Kamanda huyo wa Polisi.