Kundi la fisi limevamia kijiji cha Njoroi kata ya Ololosokwani Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha na kuua kondoo 32.
Tukio hili limetokea Ijumaa Aprili 14, 2023 katika kijiji hicho kinachopakana na pori la akiba la Pololeti na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Njoroi, James Memusi amesema fisi hao walivamia kijiji saa tisa usiku na kuanza kushambulia kondoo na kuwaua 20 na kisha kuvamia makazi ya Mshao Tukai na kuua kondoo 12.
"Hili ni tukio la kwanza kutokea fisi kuvamia usiku na kula mifugo wengi kiasi hiki," amesema.
Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Jorome Mauri amesema, "kuna wanyama wengi porini kwa nini wamekuja huku kijijini? Tunaomba uchunguzi isije kuwa kuna kichaa cha fisi."
Hata hivyo mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (Tawiri), Dk Eblate Mjingo amesema hana taarifa kamili za tukio hilo.
"Kuna wataalamu wetu wapo huko tunafuatilia na tutatoa taarifa lakini yale maeneo yapo jirani ya hifadhi hivyo inawezekana fisi kuvamia hayo maboma," amesema.
Mbunge wa Ngorongoro, Emmanuel ole Shangai amesema amepokea taarifa za tukio hilo na hadi jana kuna idadi kubwa ya mifugo imepotea na haijulikani ilipo.
"Ni kweli fisi wamevamia na kusababisha hasara kubwa kwa wafugaji kwani licha ya kuua kondoo 32 bado mifugo kadhaa imepotea," amesema.
Mkurugenzi wa mafunzo na takwimu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Edward Kohi akizungumza na Mwananchi Digital amesema matukio ya fisi kuvamia mazizi ya wafugaji inatokana na wanyama pori wengine kwenda maeneo ya mbali na fisi kuanza kutafuta chakula.
"Fisi kwa kawaida wanawinda na kula wanyamapori wengine sasa wanapokuwa maeneo ya mbali zaidi wanalazimika kutafuta chakula maeneo ya jirani na ndipo hapo wanakutana na mifugo," amesema.