Bibi kizee mwenye umri wa miaka 73, Hilda Mambugi, mkazi wa Kata ya Ibara, Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, amekutwa ameuawa nyumbani kwake na watu wasiojulikana huku chanzo kikidaiwa kuwa ni masuala ya ushirikina.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Songwe, Rashidi Ngonyani amethibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea Julai 22, 2023 majira ya saa 3 usiku.
“Siku ya tukio, majira ya saa 3 usiku, Bibi Hilda alikuwa ameuawa kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali kichwani na baadaye kupoteza maisha yake papo hapo.
“Taarifa za awali ambazo tunazo kutokana na uchunguzi wa tukio hilo ni kwamba huyu bibi anatuhumiwa kujihusisha na imani za kishirikina. Jeshi la Polisi linaendelea kuwaska watuhumiwa waliotekeleza tukio hilo la kinyama,” amesema Kamanda Ngonyani.
Aidha, Kamanda Ngonyani amewaasa wananchi kutoa ushirikiano ili kuwezesha kuwakamata wathumiwa hao huku pia akiwaasa wananchi kutojichukulia sheria mkononi kwani ni kosa kisheria.