Wakazi wa Mtaa wa Mkapa Kata ya Igoma wilayani Nyamagana mkoani Mwanza, wameiomba serikali kupeleka wataalamu wa miamba katika mtaa wao ili kupasua jiwe ambalo limezua hofu baada ya kuonekana likisogea katika makazi yao.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Ukoaji Mkoa wa Mwanza, SF Kamila Labani akikagua jiwe lililoleta taharuki kwa wakazi wa mtaa wa Mkapa, kata ya Igoma, jijini Mwanza juzi, baada ya kuanza kuhama kwenye eneo lake la asili likielekea katika makazi ya watu.
Jiwe hilo linajongea baada ya kunyesha kwa mvua kubwa huku likidondosha udongo uliokuwa umelishikilia.
Wakizungumza nasi kwa nyakati tofauti wananchi hao walisema jiwe hilo kubwa limekuwa likisogea kwenye makazi yao, kwamba limekuwa tishio kwao na watoto.
Mmoja wa wakazi hao kutoka Mtaa wa Mkapa, Farida Ramadhan alisema: “Kwanza udongo uliokuwa umelishikilia ulishushwa na mvua ambazo zimekuwa zikinyesha mara kadhaa huku jiwe lililokuwa limelishikilia nalo likaanza kupasuka, hivyo kutokana na sisi kuwa katika mteremko tunahofu jiwe hili likiachia lazima lifikie kwenye nyumba yetu na kuleta madhara”.
Mkazi mwingine wa Mtaa wa Mkapa, Philimon Ludovick, alisema njia pekee ya kulizui jiwe hilo ni kupelekwa wataalam wa miamba ili waweze kujua namna ya kuliondoa pasipo kuleta madhara, kwamba endapo likipasuliwa kawaida linaweza kuporomoka katika nyumba jirani na kusababisha hasara.
Akizungumza nasi, Mwenyekiti wa Mtaa waMkapa, Fadhil Emmanuel alisema wamefanya juhudi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kulishirikisha Jeshi la Polisi ambalo liliwashauri kuchangia fedha na kuwalipa watu wanaopasua miamba ili walipasue.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Kamila Laban, alifika katika eneo hilo na kuwataka wananchi mkoani humo kufuata sheria za ujenzi husani katika maeneo ya milimani.
Alisema: “Tumeliona jiwe hili kweli ni hatarishi na muda wowote linaweza kuporomoka na kuangukia nyumba zaidi ya saba kutokana na kuwa mlimani lakini tutaleta wataalamu wa miamba kutoka maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na wale wa migodini ili wasaidie kulipasua kabla halijaleta madhara”.