Watu wanne wamefariki dunia na wengine 37 kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha magari mawili wilayani Handeni mkoani Tanga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga (RPC), Safia Jongo amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo ambayo ilitokea usiku wa kuamkia leo Jumatano Machi 16, 2022 katika Kijiji cha Sindeni.
Kamanda Jongo amesema kuwa basi ndogo la abiria aina ya Coaster iligonga Toyota Hiace na watembea kwa miguu na kusababisha vifo vya watu wanne na majeruhi 37.
"Chanzo cha ajali hii ni gari aina ya Isuzu Jorney ikitokea Tanga mjini kwenda Handeni, iligonga watembea kwa miguu na gari ambayo iliharibika njiani ambapo watu watatu walifariki hapohapo na mmoja alifariki hospitali akiwa anapatiwa matibabu huku saba wakijeruhiwa sana na wengine wamepata michubuko " amesema
Mganga mkuu Hospitali ya mji Handeni, Dkt Hudi Shehdadi amesema kuwa walipokewa majeruhi 38 ambapo mmoja alifariki dunia akiwa bado anapatiwa matibabu.
Shuhuda wa ajali hiyo Mustapha Bakari amesema walisikia kishindo barabarani na baada ya kwenda eneo la ajali walikuta majeruhi mmoja, wakati wanaendelea kumuhudumia ghafla alisikia kishindo na kukuta wameshagongwa na gari nyingine.
Wengi wa majeruhi wa ajali hiyo ni wananchi wa kijiji cha Sindeni ambao walijitokeza kwaajili ya kushuhudia ajali ya kwanza,ambapo lilitokea basi lingine na kuwagonga wakiwa eneo la tukio.