Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Rebeca Nsemwa ametoa siku 14 kwa timu aliyoiunda kuchunguza malalamiko ya wananchi wa vijiji vya Dalla, Mbwade na Kongwa wilayani humo kuhusu mgogoro wa ardhi kati yao na mwekezaji aliyetajwa kwa jina la Luhaga Mpina.
Wananchi hao walinukuliwa na vyombo vya habari wakimuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati mgogoro huo unaohusu shamba lenye ukubwa wa ekari zaidi ya 1,000 na umedumu kwa karibu miaka 12.
Mpina hakupokea simu ya Daily News Digital alipotafutwa hata hivyo aliliambia Shirika la Utangazaji (TBC) kuwa hawezi kuzungumzia mgogoro huo. Mkuu wa Wilaya amemtaka mwekezaji huyo kutoa ushirikiano kwa timu hiyo ikiwa ni pamoja na kuwasilisha nyaraka zote zinazompa uhalali wa kumiliki ardhi inayolalamikiwa.