Jeshi la polisi mkoa wa Mwanza linamshikilia Osward Kaijage mwenye umri wa miaka 39 mfanyakazi wa mgodi wa GGM Geita, kwa tuhuma za kusababisha vifo vya watu sita na wengine kumi na sita kujeruhiwa katika ajali iliyotokea jumamosi wakati watu hao wakifanya mazoezi.
Akizungumza na waandishi wa Habari kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa amesema dereva huyo amekamatwa eneo la kisesa na bado anahojiwa na jeshi hilo pindi upelelezi utakapokamilika atafikishwa mahakamani.
Aidha kamanda Mutafungwa ametoa wito kwa vikundi vyote vinavyofanya mazoezi ya mchakamchaka kujisajiri kwenye ofisi za utamaduni katika ngazi ya wilaya, manispaa na jiji ili wapate miongozo au maelekezo ya namna bora ya kufanya mazoezi kwa kuzingatia hali ya usalama wao na watu wengine.
Katika hatua nyingine viongozi wa vikundi hivyo vya mazoezi watakutanishwa katika uwanja wa Nyamanaga siku ya Jumamosi kwa ajili ya kupewa elimu ya usalama barabarani na mambo muhimu wanayotakiwa kuzingatia wakiwapo barabarani wakati wa michezo ili kuepuka ajali.