Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

A-Z mume kumuua mke kwa risasi 7, missed call 42 za simu zatajwa

Mauaji Mwanza Mkl Ml Swalha enzi za uhai wake

Mon, 30 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Imekuwa ni simanzi kwa familia ya Swalha kufuatia tukio la mauaji ya mwanamke huyo ambaye alikuwa akijishughulisha na masuala ya urembo (make-up artist) kuuawa na mumewe aliyetambulika kwa jina la Said linazidi kuibua mambo mengi na mzito.

Usiku wa kuamkia jana Jumapili Mei 29, 2022 Swalha alidaiwa kuuawa na Said kwa kupigwa risasi 7 za kichwani nyumbani kwao, Buswelu jijini Mwanza. Taarifa kutoka kutoka kwa watu wa karibu zinasema kuwa chanzo ni wivu wa kimapenzi.

Yapo madai ambayo yamekanushwa na ndugu wa marehemu kwamba Said alimkataza Swalha asiende kwenye shoo ya msanii Diamond Platnumz, lakini akakaidi na kwenda huko.

Jamaa huyo inasemekana naye alitishia kwenda kujiua na kutokomea kusikojulikana. Hata hivyo, mama mzazi wa marehemu, Tiba Mohammed amesimulia A-Z kilichotokea kuhusu ndoa ya mwanawe huyo na mumewe ambao wamedumu kwenye ndoa kwa takriban miezi mitano; ilifungwa Desemba 30, 2021.

Mama wa marehemu anasimulia; “Watoto wangu (akiwemo Swalha) waliitwa na baba yao hapa nyumbani (Mei 28, 2022), walipofika baba yao akapata dharura hivyo hakuzungumza nao nikabaki nao tukawa tunataniana tu.

“(Swalha) alikuwa akinitania kwa kufurahi kuwafunga Simba akawa anishawishi na mimi nihamie Yanga (Yanga iliifunga Simba bao 1-0 siku hiyo kwenye Dimba la CCM-Kirumba Mei 28, 2022).

“Baadaye baba yake (baba wa Swalha) akapiga simu na kusema mume wa Swalha (Said) amepiga simu kumjulisha kuwa amefika (alikuwa safarini) na hivyo Swalha aende akampokee Igombe.

“Swalha akasema gari lake halina mafuta hivyo wakakubaliana wakutane nyumbani kwao (nyumbani kwa Swalha na Said) na mwanaume akasisitiza kuwa ana njaa sana, akamtaka mke wake aende akampikie.

“Nikawasindikiza (Swalha) hadi barabarani muda wa saa moja usiku, muda huohuo mume wake akapiga simu akiwa anafoka, nikamtaka awe na subira mkewe anakuja yupo njiani.

“Kuhusu ugomvi kati yao labda ni kuhusu simu, Jumatano iliyopita alipata tenda ya kwenda kumpodoa bibi harusi huko Shinyanga. Alipofika huko wakati akiwa kwenye kazi mume akawa anapigapiga simu, Swalha akawa anamwambia asimpigie kwa kuwa yupo kwenye kazi.

“Ijumaa jioni akawa anamtafuta hivyohivyo na kumsisitiza arudi nyumbani, Ijumaa hiyohiyo jioni akarudi, akafika nyumbani usiku, mume akawa anapiga simu, Swalha akapokea na kumwambia anaomba apumzike kwa kuwa amepodoa watu wengi na amesimama muda mrefu hivyo amechoka.

“Mwanaume akawa anaendelea kupiga simu usiku huohuo, Swalha akalala, alikuja kushtuka saa tisa usiku akakuta miss call 42. Akampigia alivyopokea wakaanza kukwaruzana tena, mwanaume akawa analalamika na kumfokea alikuwa wapi na anafanya nini mpaka hapokei simu?

“Swalha alivyoona wanazidi kugombana akaamua kuweka simu pembeni ili ugomvi usiwe mkubwa.

“Asubuhi yake mume wake akanipigia simu na kusema kuwa mke wake amemjibu vibaya. Kwa hiyo ndiyo akapanga kurudi Mwanza.

“Baba yake alivyomuita hapa nyumbani nadhani alitaka wazungumze kuhusu hilo, lakini ikatokea wamepishana na mume alivyofika nadhani ugomvi utakuwa uliendelea.

“Taarifa ni za kweli, pale ndani (wanapoishi Swalha na mumewe) kulikuwa na watoto watatu wametuambia risasi zilipigwa.

“Wanasema huyo baba (Said) alikuwa na kawaida ya kuijaribu silaha yake, mara nyingine anapiga hewani, hivyo walivyosikia mlio wa risasi wakaendelea kulala.

“Ni hadi waliposikia Swalha amepiga kelele mara moja tu, lakini risasi zikawa zinaendelea kupigwa. Mtoto mmoja akaenda kusikiliza mlangoni kwa Swalha kisha akatoka mbio kwenda kuwataarifu majirani.

“Wakaenda Polisi, kumbe yule mtoto alivyotoka tu yule baba naye (mume wa Swalha) akaondoka. Polisi walivyofika wakauchukua mwili wa Swalha.

“Taarifa za tukio sisi tulianza kuzipata kutoka kisiwani huko anapofanyia kazi (mume wa Swalha), ndipo majirani wa Swalha na askari wakaja kutoa taarifa wakisema mwanangu ana hali mbaya ameshambuliwa kwa risasi.

“Baba Swalha akaondoka na ndugu zangu kwenda huko maana nilibaki nyumbani, niliishiwa nguvu baada ya taarifa hizo, nikashindwa kwenda, saa tisa usiku wakarejea na ndipo nikajulishwa kuwa Swalha ameshafariki dunia.

“Marehemu hakuwa na mtoto na sijajua nini kinaendelea mpaka sasa. “Kuhusu huyo mume wake haijulikani yuko wapi, kwani Polisi mara ya mwisho walisema wameangalia simu yake ikaonekana yupo maeneo ya Tunza (Mwanza).”

Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ramadhani Ng'anzi ni kuwa ni kweli tukio hilo limetokea kutokana na mgogoro wa ndani wa kifamilia na mtuhumiwa ametoroka, anaendelea kusakwa kwa kuwa alitoroka baada ya tukio.

Kuhusu madai kuwa mtuhumiwa ni mtu wa usalama kama inavyodaiwa na baadhi ya watu amesema siyo kweli, ni mvuvi na anamiliki silaha yake kihalali. Jina lake halijatajwa kutokana na sababu maalum.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: