Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakimalizana na Chongolo watahamia kwa Rais Samia

Chongolo Aitaka Serikali Iumalize Mjadala Wa Bandari Wakimalizana na Chongolo watahamia kwa Rais Samia

Wed, 29 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ni dhahiri bila kificho sasa kwamba ndani ya Chama Cha Mapinduzi na serikali yake kumeibuka magenge hatari sana ambayo kwa bahati mbaya ulafi wa madaraka umeyafanya kutumia mbinu ama gharama zozote zile kuhakikisha kwamba wanashughulika na wale ambao wanawaona kama ni kikwazo kwao kufikia ndoto zao za kisiasa huku wakimkanyaga yeyote yule ambaye kwa mtazamo wao wanaona huko mbeleni atazuia rafu zao kwenye michakato ya kusaka tonge kupitia uwanja wa kisiasa.

Hiki ndicho kinamkuta Katibu Mkuu wa CCM wa sasa Ndugu Daniel Chongolo ambaye kwa siku za hivi karibuni magenge hayo yameunganisha nguvu ya fedha kuratibu na kutelekeza njama za kuhakikisha yanamuondolea sifa ya uongozi Katibu Mkuu huyo wa CCM ili hatimaye Mwenyekiti wake ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amuondoe kwenye nafasi hiyo ya Mtendaji Mkuu wa chama.

Kwa muujibu wa chanzo chetu, mbinu hizi zinaratibiwa na kufadhiliwa na baadhi ya viongozi waandamizi wa Serikali na hili linathibitika kutokana na kauli ya Katibu Mwenezi wa CCM Taifa, ndugu Paul Makonda ambayo aliitoa wiki chache zilizopita mkoani Dodoma kuwa kuna viongozi waandamizi ndani ya Serikali wanafadhili magenge ya kuwatukana viongozi wenzao ikiwemo na kumtukana Rais Samia.

Katika hotuba yake Paul Makonda aliwaonya kuwa wasipoacha michezo hiyo michafu atawataja hadharani.

Ndani ya kipindi kifupi Daniel Chongolo ametungiwa kila aina ya kashfa zikiwemo za rushwa, kujilimbikizia mali, uzinzi huku watungaji wa kashfa hizo wakishindwa kutoa uthibitisho wa yale wasemayo huku wakionekana dhahiri wanataka kumshawishi Mwenyekiti wa CCM, Samia Suluhu Hassan kumfuta kazi DC huyo wa zamani wa Kinondoni na Longido kwa kigezo cha kukosa maadili ya kiuongozi.

Jambo TV imefanikiwa kuzungumza na watu wa karibu na Daniel Chongolo kupata maoni yao kuhusu yanayomkabili Chongolo ambapo mmoja ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi kutoka Kanda ya Ziwa ameidokeza Jambo TV kuwa makundi ya wasaka Urais yamekuwa yakimuona Chongolo kama mwiba kwao kuelekea uchaguzi mkuu ujao ambapo hasira zao zimekolezwa na kitendo cha kauli za Katibu Mwenezi wa CCM Paul Makonda kuwaonya wasaka Urais kauli ambayo ilionekana kwenda na misimamo ya Katibu Mkuu Chongolo.

Mjumbe huyo ametahadharisha kuwa uroho wa madaraka ni mkubwa sana ndani ya chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu kiasi kwamba magenge hayo ya wasaka madaraka yakifanikiwa kumuondoa Katibu Mkuu Chongolo wataanza rasmi mapambano dhidi ya Mwenyekiti wa sasa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanauona huu kama mtihani mkubwa unaomkabili Rais Samia kuelekea kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa inayotarajia kuketi leo Novemba 29, 2023 Jijini Dar es Salaam ambapo nafasi ya Chongolo kuendelea kuwa Mtendaji Mkuu wa CCM itaamriwa.

Endapo Mwenyekiti atafanya mabadiliko kwenye nafasi hiyo kutaibuka hisia ya kwamba kundi linalofadhili utengenezwaji wa tuhuma dhidi ya Chongolo litakuwa limefanikiwa hivyo kuanza kwa mapambano mapya dhidi ya Mwenyekiti wao kuelekea uchaguzi Mkuu.

Je, nini kitatokea? Je, Chongolo anaweza kuwashinda wasaka urais? Je, Mwenyekiti Samia Suluhu Hassan atabariki ukatili huu dhidi ya Katibu Mkuu wake? Muda ni shahidi mzuri.

Na John Marwa

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: