Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi – CCM, Daniel Chongolo amesema Tanzania ipo katika mapambano ya vita vya kiuchumi na amewataka Watanzania kuwa makini na watu wachache wenye dhamira ovu ya kutumia mjadala wa uwekezaji bandarini kuvuruga amani iliyopo, kwa sababu wanapo pa kukimbilia nje ya nchi, kama baadhi yao walivyofanya miaka michache iliyopita.
Chongolo ameyasema hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara mjini Korogwe, Tanga, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake, kufafanua na kuwaelimisha wananchi masuala mbalimbali yanayotekelezwa na Serikali kupitia Ilani ya CCM, ikiwemo suala la makubaliano ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai ya kuanzisha ushirikiano na uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam.
Amesema, ingawa uhuru wa nchi ulipatikana baada ya kuwaondoa wakoloni, mapambano ya kujikomboa kiuchumi yako katika changamoto ya vita vya kiuchumi ambavyo havionekani kwa macho, lakini vinahitaji akili, busara na mikakati zaidi kuvipigana na kwamba nchi inatakiwa kuwa imara, ili isiyumbishwe na maadui wasioitakia mema.
“Niwaambie miaka ya 50 kwenda ya 60 tulipigania uhuru wa nchi yetu. Uhuru ulipatikana na sasa Tanzania iko huru. Lakini vita haijaisha. Vita inaendelea. Sasa hivi hatupiganii uhuru tena. Kwa sababu upo. Vita ya sasa ni vita ya uchumi. Na hii ni vita ya dunia. Na sisi Tanzania ni sehemu yake. Na sisi tunapigana vita hiyo, asubuhi mchana na jioni. Ndugu zangu wana-Tanga, vita ya uchumi ni vita ya kutumia akili, busara na ya kimkakati zaidi.”
“Huwezi kuiona kwa macho, hauwezi kuishika kwa mkono. Lakini ni vita tena ni vita kubwa, kuliko ile ukombozi wa wakati huo. Ni vita ambayo ukikaa kienyeji umeenda na maji. CCM hoyee…CCM hoyee…Vita hii ukikaa kienyeji umeenda na maji. Kwanini nasema ukikaa kienyeji umeenda na maji? Kwa sababu fursa tunazopigania wote, kuzipata na kuzitumia ili kujiendeleza ni fursa za aina moja na zinapatikana kwenye maeneo yale yale. Kwa hiyo kila mmoja anaiangalia fursa kwa jina lake, kwa jicho lake, kwa namna yake na kwa mazingira,” amesema Ndugu Chongolo.
Aidha, amesisitiza kuhusu umuhimu wa Watanzania kuilinda amani, amesema kuwa hiyo ni mojawapo ya tunu ambazo waasisi wa Tanzania walihakikisha inakuwa ni utambulisho wa taifa na inatakiwa kulindwa na kutetewa kwa nguvu zote bila kuwaonea aibu wala kuwaogopa wote wanaotishia kuivuruga kwa maslahi ya kisiasa.
“Mwalimu Nyerere (Baba wa Taifa), alisema ukiulizwa Tanzania una nini, sema una amani huku ukijidai. Amani hii si amani rahisi, si amani ya lelemama, kuna watu wametoka jasho na wanatoa jasho ili hii amani iwepo. Tusiache amani hii ipotee kwa sababu ya wajanja wachache wenye dhamira ovu kwa nchi yetu, wenzetu wana mahali pa kukimbilia.”
“Na ushahidi tumeuona miaka michache iliyopita. Walivyoona huku mambo yao yamekaa vibaya walitafuta pa kuishi. Sisi tuna wapi pa kukimbilia nje ya Tanzania? Kama hatuna tujue tuna wajibu wa kuilinda amani ya nchi hii, tuna wajibu wa kuiendeleza nchi hii. Na tuna wajibu wa kusimamia maslahi ya nchi hii bila aibu wala kumuogopa yeyote,” amesema Ndugu Chongolo akisisitiza pia kuwa CCM itahakikisha maoni ya wananchi yenye tija na chanya, yanafanyiwa kazi na Serikali katika hatua za kuingia mkataba wa utekelezaji.