Aliyekuwa Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Simai Mohammed Said leo amehojiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) katika vikao viwili tofauti.
Simai, mwakilishi wa Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja, alijiuzulu wadhifa huo Januari 25, 2024 akisema mazingira ya kazi si rafiki.
Siku mbili kabla ya kujiuzulu nafasi yake, Simai alikutana na wadau wa utalii akasema sekta hiyo imeanza kupata changamoto baada ya kukosekana vileo Zanzibar.
Simai alitaja sababu kubwa ya changamoto hiyo ni kubadilishwa kampuni za kuingiza vileo kisiwani humo, akiilalamikia Bodi ya vileo Zanzibar kuchukua uamuzi huo bila kuishirikisha wizara yenye dhamana ya utalii.
Katika picha jongefu iliyowekwa mitandaoni, akiwa amevaa sare ya CCM, Simai amesema ni vikao vya kawaida kwenye chama hicho, lakini yeye si msemaji wake.
Alipotafutwa na Mwananchi Digital, amekiri kuitwa na chama hicho, lakini hakuwa tayari kuzungumzia alichoitiwa na kilichojiri, badala yake ameelekeza watafutwe wahusika.
Akizungumza jana Januari 6, 2024, Katibu wa CCM Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja, Omar Morrice amesema mwakilishi huyo ameitwa na vikao viwili katika ngazi ya jimbo na wilaya.
Bila kuingia kwa undani juu ya sababu za kuitwa na mazungumzo ya vikao hivyo kwa madai kwamba ni vya ndani, Morrice amesema ni haki ya chama na mwanachama mwenyewe kukutana wakazungumza.
“Ni kweli ameitwa kwenye chama na mimi ndiye mratibu wa vikao hivyo, kwani kuna shida gani, Simai ni mwanachama halali wa Chama cha Mapinduzi, kwa hiyo chama kimemuita mwanachama wake wazungumze, kuitana mkazungumza mambo fulani fulani hiyo ni haki ya chama, lakini ni haki ya mwanachama mwenyewe,” amesema.
Amesema asubuhi ya jana Simai aliitwa katika kikao cha jimbo na mchana akaitwa katika kikao cha wilaya.
Alipoulizwa ni hatua gani zitafuatwa au kuendelea kuitwa katika vikao vingine vya juu, Morrice amesema hawezi kuzungumzia ya mbele. Ilivyokuwa
Wakati akiwaapisha mawaziri na naibu mawaziri akiwamo Mudrick Ramadhan Soraga aliyechukua nafasi ya Simai Februari mosi, 2024 Ikulu Zanzibar, Rais Hussein Mwinyi aliwataka mawaziri wanapotaka kuwajibika, wakijiuzulu waseme ukweli.
Alisema kujiuzulu ni njia ya kuwajibika, kwa hiyo iwapo kuna waziri anaona kuna sehemu hakubaliani na Serikali katika maamuzi ni vyema akasema na ataheshimika zaidi.
“Wakati unawajibika, lazima uwe mkweli na ukweli ninaousema hapa lazima kama kuna mgongano wa masilahi uutangaze,” alisema.
Alisema ikiwa kuna sababu yoyote inayomfanya mtu ajiuzulu anawajibika kuwa wazi na kusema: “Kama tumezuia kitu na wewe una biashara hiyo tangaza, sema ukweli, sema hapa kuna mgongano wa masilahi mimi ni muagizaji wa kitu fulani na ninyi mmezuia, kwa hiyo tuwe wakweli.”
Baada ya Kauli ya Rais Mwinyi, Simai alisema kiutamaduni si busara kuhoji, kujibu kuongeza au kupunguza kauli ya Rais labda ingekuwa ndani ya vikao vya chama au Baraza la Mapinduzi.
Hata hivyo, alisema Rais alisisitiza kusema ukweli wakati wa kujiuzulu jambo ambalo alilifanya.
“Kweli ni kwamba nilimpa barua kujiuzulu, kweli kwamba imani yangu ni kuwa mazingira ya kazi kwa upande hayakuwa yakinipa uwezo kusimamia sekta hii muhimu kwa uhai wa uchumi wa Zanzibar kwa kiwango ambacho ningependa kuona nafikia,” hii ni sehemu ya maneno ya Simai aliyoongea baada ya kauli ya Rais Mwinyi.