Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nchimbi awaonya viongozi wa CCM wasiowajibika

Nchimbi Ccm (22).jpeg Nchimbi awaonya viongozi wa CCM wasiowajibika

Thu, 22 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

​​​​​​​Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema viongozi wanaotokana na chama hicho wanaoshindwa kutimiza wajibu wao wa kutumikia wananchi, siku zao zinahesabika na kwamba hakitawavumilia.

Amesema viongozi wote wanaotokana na CCM wanatarajiwa kuwa watumishi wa wananchi waliowachagua, wakiwatumikia kwa nguvu zao zote, wakiweka maslahi ya umma na Watanzania mbele wakati wote, kabla ya masuala yao binafsi.

Dk. Nchimbi amesema hayo alipokuwa akisisitiza namna bora ya kumuenzi Hayati Balozi Dk. Diodorus Kamala, kupitia salamu za pole na rambirambi za CCM wakati wa kuaga na kutoa heshima za mwisho kijijini kwao Rwamashonga, Jimbo la Nkege,  Misenyi mkoani Kagera.

Mbali na salamu za CCM, Balozi Nchimbi pia amewasilisha salamu maalum za rambirambi kwa wafiwa na waombolezaji wote kisha mkono wa pole kwa familia ya Hayati Dk. Kamala, kutoka kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye alieleza namna alivyoguswa na msiba huo.

Dk. Nchimbi amesema moja ya uwezo mkubwa aliokuwa nao Dk. Kamala ni pamoja na saikolojia ya kutafuta suluhisho la changamoto za watu tangu alipokuwa Rais wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe.

Pia amemwelezea kuwa alikuwa mwadilifu, aliyechukia rushwa kwa vitendo, kiasi cha kuwa tayari kugharimu na kupoteza ubunge wa Nkenge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 kwa sababu hakuwa tayari kupokea fedha kuwasaliti wananchi wa jimbo hilo, aliokuwa anawatetea kwenye changamoto zao.

“Kamala hakuwa mla rushwa. Hili naweza kulisemea kwa kiapo. Hata alipopoteza ubunge, hakuwahi kulalamika kwa sababu alijua zile zilikuwa hela za udhalimu, hela za usaliti kwa wananchi wake. Watu wa namna hii lazima tuwaenzi vizuri kwa kutambua mchango wao mkubwa," amesema Balozi Dk. Nchimbi.

"Hongereni sana Misenyi kwa kuwa na Mwana wa Afrika wa namna hii. Mjisikie fahari sana. Nimefurahi kusikia Mwenyekiti wa Halmashauri na Mbunge wa sasa (Jimbo la Nkenge) walivyoelezea mambo aliyofanya Dk. Kamala na walivyo tayari kuyaendeleza na kufanya zaidi.

“Viongozi tunayo mengi ya kujifunza kwa watu kama Dk. Kamala. Vijana mnayo mengi ya kujifunza kwake hasa kutimiza wajibu kwa kuwatumikia wananchi, kuweka maslahi ya nchi na kuwa na msimamo thabiti bila kigugumizi kwenye maslahi ya nchi. Na sisi CCM wajibu wetu tutawatetea na kuwalinda viongozi wanaotumikia wananchi na kutimiza wajibu wao," amesema.

Kadhalika, Balozi Nchimbi amesema viongozi wachache ambao bado wanasuasua katika kutumikia wananchi, wanatakiwa kuongeza juhudi.

"Wale viongozi wachache wanaotanguliza maslahi yao binafsi mbele, ambao hawatimizi wajibu wao kuwatumikia wananchi, siku zao zinahesabika. Tunatakiwa kuwatumikia wananchi kwa nguvu zetu zote.

“Dk. Kamala alikuwa na msimamo usioyumba kusimamia maslahi ya nchi. Kwenye vikao vya kimataifa, linapokuja suala la kutetea maslahi ya Tanzania, Kamala hakuwa na kigugumizi hata kidogo.

“Alikuwa na uwezo wa kusema bila kuangalia anaowakatalia wanatoka mataifa gani na watamfikiriaje, alikuwa hamwangalii mtu usoni anatokea wapi. Alikuwa na madhaifu yake kama binadamu lakini yanazidiwa na uwezo na nguvu,” amesema.

Dk. Kamala, ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Nkenge kwa nyakati mbili tofauti, kabla ya kuwa Naibu Waziri na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki kisha Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Luxembourg na Jumuiya ya Ulaya, mjini Brussels, alifariki dunia  Februari 12, mwaka huu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: