Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makonda awaita upinzani uwanjani, Chadema yajibu mapigo

Msafara Wa Makonda Wasimamishwa Ilemela Makonda awaita upinzani uwanjani, Chadema yajibu mapigo

Tue, 14 Nov 2023 Chanzo: Mwananchi

Wakati Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Paul Makonda akivitaka vyama vya upinzani vifanye mikutano ya hadhara ili washindane katika majukwaa, baadhi ya viongozi wa Chadema wamekutana jijini Arusha kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kupanga mikakati ya mashambulizi.

Akizungumza Novemba 13 wilayani Magu mkoani Mwanza katika mfululizo wa mikutano yake katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, Makonda amesema amechoka kutamba peke yake, huku akivitaka vyama alivyoviita vya watoa taarifa kutumia fursa waliyopewa na Rais Samia Suluhu Hassan kufanya mikutano ya hadhara.

“Ndugu zangu kina Mbowe (Freeman) na Lissu (Tundu) na wengine inawezekana wana mawazo mazuri, tutayapokea mawazo yao kwa sababu tunaye Rais Samia aliyekata Tanzania kuwa na umoja na kila mtu ana haki sawa.

“Changamoto walioipata ndugu zangu (Chadema) wameishiwa mafuta ya helikopta, nimeshawaombea kwa Rais Samia ili kuendelea na mikutano yao ya hadhara,” amesema Makonda.

Amesema amechoka kutamba peke yake katika majukwaa, akisema angefurahi kuona vyama vingine vikifanya mikutano ya hadhara.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itikadi, Uenezi wa Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alipoulizwa na Mwananchi kuhusu kauli za Makonda, amesema kiongozi huyo anatafuta sifa kupitia Chadema.

Ameongeza kuwa Chadema imeshafanya mikutano zaidi ya 100 Kanda ya Ziwa ikiwemo maeneo ya vijijini.

"Huwa hatupendi kubishana au kujibizana na huyu, tunamuona mara amepanda farasi, baiskeli, lori sasa asitafute 'kiki' kutoka kwetu," amesema Mrema.

Kuhusu matumizi ya helkopta, Mrema amesema, "mwambie suala la chopa Makonda halimhusu kama anaitaka na yeye atafute ya kwake.

Katika hatua nyingine baadhi ya viongozi wa Chadema wamemaliza kikao chao cha faragha jijini Arusha kujadili masuala kadhaa ya chama hicho.

Kikao hicho cha siku mbili cha faragha kiliongozwa na Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe pia alihudhuria Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tundu Lissu, John Heche, Ezekiah Wenje na Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa na Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema.

Kikao cha viongozi hao wa Chadema kimekuja zikiwa zimepita wiki mbili tangu mikutano yao ilipositishwa katika Mkoa wa Songwe kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kukosekana kwa helkopta baada ya kutokea mvutano kati yao na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).

Akizungumza nasi jana, Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Aman Golugwa alisema kikao hicho kimefanyika na kumalizika vizuri juzi. "Ni kweli viongozi wa kitaifa walikuwa na kikao cha ndani hapa Arusha na iliwalazimu kukutana Arusha kwa sababu ya wito wa Polisi kwa Makamu Mwenyekiti Lissu ambaye alilazimika kurudi nchini," amesema Golugwa Hata hivyo, Golugwa amesema kikao hicho, kilikuwa cha faragha cha viongozi wakuu na Wajumbe baadhi wa Kamati Kuu tu. Mbali na Chadema, wiki hii Kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe anatarajiwa kuwa ziara ya siku 10 katika majimbo nane ya mkoa wa Kigoma.

Chanzo: Mwananchi
Related Articles: