Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Balozi Karume awekwa chini ya uangalizi CCM

Karume Ccm Kuhojiwa Balozi Karume awekwa chini ya uangalizi CCM

Wed, 28 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimemuweka chini ya uangalizi wa miezi mitatu kada wake Balozi Ali Abeid Karume kutokana na kauli zake za kukidhalilisha chama na viongozi wake.

Hatua hiyo inatokana na onyo alilopewa na kamati ya siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Jimbo la Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja iliyokutana Juni 15, 2023.

Karume aliitwa kuhojiwa na kamati ya maadili ya jimbo hilo kutokana na kauli zake alizozitoa kwenye mitandao ya kijamii akikituhumu chama kuwa hakijawahi kushinda kihalali kisiwani humo na kumkosoa hadharani Rais Hussein Mwinyi kuhusu sera zake za kukodisha visiwa.

Pia alipinga utaratibu wa wananchi wa Kilimani kuondolewa kujenga ukumbi wa kimataifa na ujenzi wa uwanja wa Amani akidai vinakiuka utaratibu.

Kwa mujibu wa barua ambayo Mwananchi limeiona iliyosainiwa na Katibu wa CCM jimbo la Tunguu, Sharifa Maabadi Othman, bila kutaja muda, inaeleza chama kumpa onyo hilo kwa kukiuka maadili.

“Pamoja na mambo mengine kikao kilipokea taarifa kutoka kamati ya maadili ya jimbo kuhusu mahojiano yaliyofanyika juu ya Ali Abeid Karume na kamati ya maadili ya jimbo, pamoja na makosa yake aliomba msamaha katika kikao hicho, kimeamua kukupa onyo kwa kukiuka maadili ya chama chetu,” inaeleza sehemu ya barua hiyo.

Hata hivyo, Mwananchi lilipomtafuta katibu huyo Sharifa kuhusu hatua hiyo, licha ya kusema hawezi kuzungumza chochote kwa sababu yaliyofanyika ni vikao vya ndani, alikiri barua hiyo ni halali.

Balozi Karume alipotafutwa juzi na jana hadi saa 6:50 mchana alisema bado hajapokea barua yoyote kutoka kwenye chama hicho tangu walipomaliza kikao chao.

Hata hivyo, alisema naye ameona barua hiyo kwenye mtandao wa kijamii, akasema ikimfikia atatii maadili ya chama.

Balozi Karume alihojiwa na kamati ya maadili ya tawi la Mwera, kamati ya maadili ya Jimbo la Tunguu na kamati ya maadili ya Wilaya ya Kati.

Barua aliyopewa Karume ni kwa mujibu wa kanunzi za uongozi na maadili za CCM na jumuiya yake toleo la mwka 2021 ibara ya (8) kifungu kidogo (a) (ii).

Nakala ya barua hiyo ilikwenda kwa Katibu wa CCM wilaya ya Kati na Katibu wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja.

Kutokana na kanuni hiyo mwanachama anayekiuka maadili ya chama anapewa onyo, onyo kali au kufukuzwa uanachama huku kukiwa na muda maalumu wa uangalizi kuanzia miezi mitatu, sita na mwaka mmoja.

Mmoja wa watu wa ndani ya chama hicho ambaye hakutaka kutajwa alisema iwapo kikipita kipindi cha uangalizi bila kuonyesha maabdiliko, wilaya itatoa mapendekezo kwenda ngazi ya mkoa kwa hatua zaidi.

Mapendekeo hayo yanaweza kuwa kumfukuza uanachama kiongozi huyo.

Akizungumza na gazeti hili mchambuzi wa masuala ya kisiasa Zanzibar, Ali Makame alisema hatua iliyochokuliwa ni sawa kwa sababu lengo la kila chama ni kuishika dola, lakini kuna taratibu za kufuata katika kuzungumza.

“Ukiangalia huyu ni mtoto wa muasisi wa taifa hili na chama chake, kwa hiyo anajua mengi, madhaifu na mazuri ya chama, lakini kutoka hadharani na kuanza kusema vile si uungwana, kama unapinga tumia utaratibu wa chama unapotoka nje unakuwa utovu wa nidhamu,” alisema

Hata hivyo, alisema hatua zilizochukuliwa na chama hicho ni jambo la kujifunza hata kwa watu wengine kwa sababu linaweza kuwagawa wanachama na viongozi, hivyo kuwaondoa kwenye lengo la chama kama kikundi chenye dhamira moja.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: