Serikali imesema katika kipindi cha Februari hadi Machi, 2023, watu 72 wameugua ugonjwa wa kipindupindu na wengine watatu wamefariki dunia katika mikoa minne, huku ikizindua mpango shirikishi wa taifa wa kuzuia na kukabili.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene, aliyasema hayo jana alipokuwa akizindua mpango huo jijini hapo.
Simbachawene alisema ugonjwa huo uligundulika Februari 19, hadi Machi 15, 2023, wamepokea taarifa ya wagonjwa 60 ambao kwa Mkoa wa Ruvuma ni 13, Kigoma (7), Katavi (34) na Rukwa (18).
“Tanzania ilishuhudia kipindi kirefu cha mlipuko wa kipindupindu hapa nchini kuanzia mwaka 2015 hadi 2018. Mlipuko huo ulitupa uzoefu mkubwa katika kukabiliana na ugonjwa huo hatari.
Hata hivyo, mlipuko wa ugonjwa huu umepungua katika sehemu kubwa ya nchi yetu,” alisema.
Akizungumzia mpango huo, Simbachawene alisema ulifanyiwa mapitio na utaiwezesha serikali kuimarisha shughuli za uratibu na kuweka mifumo madhubuti ya kisekta ya kukabiliana na ugonjwa huo hatari.
“Huu mpango utaziwezesha wizara zinazohusika, Idara, Taasisi, Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa kushiriki kikamilifu katika hatua za kuzuia, kujiandaa kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu na kurejesha hali pindi ugonjwa huo unapotokea,” alisema.
Hata hivyo, alisema katika tathmini iliyofanyika ya ugonjwa huo ilitaja sababu za kujirudia kwa milipuko kwenye maeneo mbalimbali unaotokana na ukosefu wa majisafi na salama kwa jamii husika, uelewa mdogo wa namna ya kujikinga na kupambana na ugonjwa huo na jamii kukosa vyoo bora na matumizi hafifu ya vyoo.
Kadhalika, alisema taarifa kutoka Shirika la Afya Dunia (WHO) inaeleza kuwapo na mlipuko mkubwa wa kipindupindu nchini Malawi na hadi kufikia Machi 15, 2023 kulikuwa na jumla ya wagonjwa 53,925 na vifo 1,658 vilivyotolewa taarifa.
“Taarifa hii inatupa tahadhari ya mlipuko huo pia kuvuka mipaka na kuingia nchini kwetu hususani pale tusipo imarisha afua mbalimbali za kujikinga na kipindupindu kwa jamii zetu hususani kwa mikoa inayopakana na nchi hiyo, tetesi za kuwapo kwa mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu pia zipo kwa nchi nyingine tulizopakana nazo kama Msumbiji, DRC Congo, Zambia na Kenya,” alisema.
Aliihimiza Wizara ya Afya kuongeza nguvu ya ufuatiliaji ili kuhakikisha wagonjwa na tetesi zote zinatolewa taarifa na kutibiwa mapema kwenye vituo vya kutolea huduma kabla ugonjwa haujsambaa kwenye maeneo makubwa zaidi.
“Naelekeza Ofisi za tawala za Mikoa na Halmashauri zote kushirikiana na mamlaka za maji mijini na vijijini (RUWASA), ili kuhakikisha hali ya upatikanaji wa maji katika maeneo yao inaimarika,” alisema.