Kesi za ndoa na talaka zinazopelekwa katika mabaraza ya usuluhishi ngazi ya kata zimegeuka tishio Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, ikielezwa kundi lililoathirika zaidi na migogoro hiyo ni la miaka 35 hadi 50.
Aidha, inaelezwa wanandoa hao wanapokwenda katika mabaraza hayo, wengi wao huwa tayari walishachukua uamuzi mgumu wa kujiandika talaka na wanapofika barazani, huwa hawataki usuluhishi zaidi ya fomu namba tatu ya Mahakama inayohusu takala.
Wajumbe hao walifichua siri hiyo wakati wa mafunzo yaliyoandaliwa na Shirika la KWIECO, linaloendesha mradi wa majaribio wa utatuzi na usuluhishi wa migogoro ya kifamilia, nje ya vyombo vya Mahakama na polisi, unaotumia njia mbadala za utatuzi na usuluhishi wa migogoro (ADR).
Mradi huo unafadhiliwa na Shirika la Legal Service Facility Tanzania (LSF). Mjumbe wa Baraza la Usuluhishi Kata ya Uru Kusini, Aurelia Njau, akizungumzia changamoto hiyo alisema:
“Wanakuja kwetu wakiwa tayari kila mtu ameshaanda hatma yake kwamba hapa tumefikia hitimisho, hatutaki tena ndoa. “Kwa hivyo, kila unapomsuluhisha unamwambia kubalianeni pale mlipotoka, mlipoanzia mapenzi yenu hebu jaribuni kujishusha.
Ukimwambia kaka jishushe au dada jishushe, anakupa karatasi, anakwambia hapa ndoa ni mapenzi, hakuna tena mwanzo, wala mwisho, tumefikia mwisho.
Aidha, mjumbe mwingine wa baraza la usuluhishi, Flomena Kway, alisema hivi sasa wanapitia wakati mgumu, kwa kuwa wanandoa wanaokwenda kwenye mabaraza hayo hawataki kusuluhishwa na kuridhiana, wao lengo lao kuu ni talaka.
Akitoa maelezo kuhusu mafunzo hayo, Mratibu wa Mradi wa ADR, Lilian Mandari, alisema hadi kufikia sasa wameshawafikia wasaidizi wa kisheria 173, kwa sasa wanaendelea kutoa elimu hiyo kwa mabaraza ya kata.
Baada ya maelezo hayo, Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Muhsin Kilua, aliwaeleza wajumbe hao kuwa, mfumo huo wa utatuzi wa migogoro una manufaa kadhaa ikiwa ni paamoja na uwepo wa taratibu rafiki na rahisi kwa mlalamikaji na mlalamikiwa, migogoro kumalizwa kwa maridhiano na kutatuliwa kwa muda mfupi.
Awali akifungua mafunzo hayo, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la KWIECO, Peter Mashingia, alisema wanatamani kuona wajumbe hao wa mabaraza wanachaangia kuwapo kwa ongezeko la utatuzi wa migogoro ya kifamilia kwa kutumia mfumo wa ADR kwa ufanisi.
Alisema: “Maana yake ni kwamba kama takwimu za mwaka jana mlikuwa mmefikia watu 100, tunatamani kuona wale ambao wana ile migogoro inatatuliwa kwa haraka katika hizo siku 30. Na hilo ongezeko lake linaonekana kwa takwimu ambazo ziko ndaani ya kata”.