Baraza la kijeshi lililoundwa na wanajeshi waliofanya mapinduzi nchini Niger limeomba msaada wa kijeshi wa kundi la Wagner lenye mfungamano na Russia ili kukabiliana na uwezekano wa uingiliaji kijeshi wa kigeni.
Hayo yameripotiwa na shirika la habari la Associated Press ambalo limemnukuu Wasim Nasr, mwandishi wa habari na mtafiti wa taasisi ya Magharibi ya "Sofan Center" akidai kwamba wanajeshi waliofanya mapinduzi huko Niger wameomba msaada wa kijeshi wa kampuni binafsi ya ulinzi ya Wagner sambamba na kukaribia kufikia mwisho muda uliotolewa na ECOWAS wa kumwachilia huru rais "Mohammed Bazoum" na kukabidhi madaraka.
Wasim Nasr ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba Jenerali Salifou Modi, mmoja wa viongozi wa mapinduzi ya kijeshi ya Niger, hivi karibuni alitembelea Mali na kuwasiliana na afisa wa kampuni ya Wagner. Amedai kuwa, kundi la Wagner limeamua kuchunguza ombi la wanajeshi wa Niger la kulisaidia kukabiliana na uvamizi wa kigeni.
Siku chache zilizopita, wakuu wa kijeshi wa Afrika Magharibi wamekubaliana na mpango wa kuingilia kijeshi Niger wakati muda waliowapa wanajeshi waliofanya mapinduzi utakapomalizika.
Kamishna wa ECOWAS, Abdel-Fatau Musah amenukuliwa na vyombo vya habari vya kieneo na kimataifa akisema mjini Abuja Nigeria kwamba: "Hatimaye mambo yote yanayohusiana na uingiliaji wa aina yoyote ile yamefanyiwa kazi; ikiwa ni pamoja na rasilimali zinazohitajika pamoja na jinsi na lini tutapeleka kikosi (huko Niger)."
Siku ya Jumapili, Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) iliwapa wanajeshi waliompindua Rais Mohamed Bazoum muda wa wiki moja kumrejesha madarakani Bazoum au wakubali kukabiliana na matumizi ya nguvu dhidi yao. Wanajeshi hao walifanya mapinduzi hayo ya kijeshi terehe 26 mwezi uliopita wa Julai.
Wakuu wa jeshi la ECOWAS walikuwa wamekutana katika mji mkuu wa Nigeria Abuja kujadili njia za kukabiliana na mzozo huo.
Juzi Jumamosi, Baraza la Seneti la Nigeria lilimshauri rais wa nchi hiyo, ambaye ni mkuu wa hivi sasa wa ECOWAS, atafute machaguo mengine bora kulinga kutumia nguvu za kijeshi kuirejesha madarakani serikali iliyopinduliwa ya Niger. Baraza hilo lilisema kuna uhusiano wa karibu sana baina ya wananchi wa Niger na Nigeria na hilo ni muhimu kuzingatiwa kabla ya kuchukuliwa hatua yoyote ile.