Mtu mmoja mfuasi wa matambiko, Ifasoji Ayangbesan (35), amefichua jinsi alivyonunua miguu miwili ya binadamu kwa bei ya Naira 20,000 baada ya kukamatwa kwa madai ya kumuua na kumkata vipande Oyindamola Adeyemi, nchini Nigeria.
Ayangbesan, alikamatwa na washukiwa wengine 12 katika Makao Makuu ya Polisi, Eleweran yaliyopo mji wa Abeokuta na kusema miguu hiyo aliipata kwa rafiki yake Lukman, ambaye naye alidai aliikata baada ya kufukua sehemu ya mwili kutoka kaburini.
Ayangbesan ambaye ni mkazi wa mhimili wa Iloti, serikali ya mtaa Ijebu-Ode huko Ogun, alidai yeye ni mganga wa mitishamba na si mtu wa matambiko huku akikiri kununua miguu hiyo ya binadamu lakini alikana kuhusika na mauaji ya mtu huto ambaye aliripotiwa kuuawa Januari 28, 2023.
Amesema, “nilinunua miguu miwili mibichi ya binadamu, lakini sikuhusika katika mauaji ya mwathiriwa. rafiki yangu Lukman aliniambia ana jozi ya miguu ya kuuza. Ingawa nilimwambia sikuzihitaji, alinishawishi kuzitumia kwa tambiko ili kuboresha kazi yangu, nami nikakubali.”
“Nilimwambia sijui kufanya matambiko ya pesa yeye akanielekeza kwa rafiki yake Oye Egbeji wa Isiwo naye akanifundisha jinsi ya kufanya nikachoma miguu na kuiweka nyumbani kwangu nikiwa na mipango ya kukamilisha ibada nikitoka Ajah,” amesimulia Ayangbesan.
Aidha, mtuhumiwa huyo amefafanua kuwa, “binti yangu alinipigia simu kuwa polisi wamekuja kunitafuta kwa hiyo niliingia kinyemela kuchukua miguu iliyoungua ili nisikatwe na ushahidi kwa sababu nilisikia kuwa Lukman amekamatwa na ametaja ushiriki wangu katika kesi hiyo.”
Kamishna wa Polisi katika jimbo la Ogun, Olanrewaju Oladimeji, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kukamatwa kwa watu hao kunatokana na jitihada za pamoja za kukabiliana na wahalifu katika jimbo hilo, baada ya kuelezwa hali ya uhalifu wa eneo husika.