Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2024/25 iliyoanza Agosti 16, itaendelea tena keshokutwa, Jumatano kwa michezo mbalimbali ya baadhi ya mechi za raundi ya pili, pamoja na kuanza kwa raundi ya tatu.
Timu 16 zitamenyana kwa msimu mzima kusaka Bingwa wa Tanzania Bara ambaye ataiwakilisha nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu ujao.
Mbali na bingwa, timu itakayomaliza nafasi ya pili itapata nafasi sawa kama ya bingwa, kwa kuiwakilisha Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na pointi za nchi zilizopo kwenye Shirikisho la Soka Afrika, CAF.
Katika Ligi Kuu Tanzania Bara, nafasi ya tatu inachulikuwa na timu ambayo moja kwa moja inakwenda kuiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Miaka ya hivi karibuni nafasi ya nne imekuwa ikisakwa sana na timu za Ligi Kuu kwa sababu imekuwa na faida tofauti na huko nyuma.
Ni kwamba timu yoyote inayomaliza nafasi hiyo inaombea timu itakayotwaa ubingwa wa Kombe la FA, iwe moja kati ya zile zilizomaliza nafasi tatu za juu. Kwa sababu ndiyo kitu pekee ambacho kitakachoifanya timu hiyo kucheza michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mfano msimu huu, Coastal Union imecheza Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kushika nafasi ya nne kutokana na Yanga kutwaa kombe hilo wakati huo huo ndiyo Mabingwa wa Tanzania Bara ambao wanakwenda kucheza Ligi ya Mabingwa.
Kanuni zinasema bingwa wa Kombe la FA ataiwakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, lakini kama itakuwa ndiyo timu iliyotwaa ubingwa wa Ligi Kuu, basi nafasi hiyo itakwenda kwa timu iliyomaliza nafasi nne za juu kwenye Ligi Kuu.
Kitu pekee ambacho kinaifanya timu inayoshika nafasi ya nne isicheze Kombe la Shirikisho Afrika ni ubingwa wa FA kuchukuliwa na timu itakayoshika kuanzia nafasi ya tano kwenye Ligi Kuu kushuka chini, au timu za madaraja ya chini.
Kutokana na hali hiyo pamoja na ubingwa, timu 16 zinasaka nafasi nne za juu kwa ajili ya kutaka nafasi ya kucheza kimataifa.
Kwa kuzingatia hilo, katika makala haya tunakuletea timu nane zinazopewa nafasi kubwa zaidi ya kumaliza nafasi nne za juu msimu huu, twende sasa...
5# KMC
Ilibaki kidogo icheze Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita, baada ya kumaliza nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu nyuma ya Coastal Union iliyokwenda kuiwakilisha nchi katika michuano hiyo.
Ikumbukwe kuwa KMC ina vinasaba vya kucheza michuano ya kimataifa kwani ilishawahi kufanya hivyo mwaka 2019, ilipocheza Kombe la Shirikisho, ikakipiga dhidi ya AS Kigali ya Rwanda, Agosti 10 ugenini na kulazimisha suluhu, kabla ya kutolewa ikiwa nyumbani Agosti 23, mwaka huo.
Kocha Mkuu, Abdihamid Moalin, amefanya usajili mkubwa msimu huu, kwa wachezaji mbalimbali kutoka Burundi, Rwanda, na Uganda, hivyo ni moja kati ya timu zinazotarajiwa kumaliza ndani ya nne bora msimu huu.
5# Singida Black Stars
Ni moja kati ya timu iliyosheheni wachezaji wengi wa kigeni kwenye ubora mkubwa na maarufu ukiziondoka klabu za Simba na Yanga.
Inaonekana kama haitaki utani msimu huu kwani imeshinda mechi zake mbili ilizocheza mpaka sasa, tena ikiwa ugenini.
Iliichapa KenGold mabao 3-1 na kushinda bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar, na inazidiwa mabao ya kufunga na Simba tu ikiwa kwenye nafasi ya pili.
3# Azam FC
Licha ya kwamba haijawahi kutinga hatua ya makundi katika michezo ya kimataifa, lakini Azam FC, ni moja kati ya timu ambazo hazijawahi kukosa kucheza michuano hiyo, tangu Tanzania ilipoanza kuingiza timu nne kwenye michuano ya kimataifa.
Pamoja na kutofanya vema, lakini haiondoi kuwa ni timu yenye msuli mkubwa linapokuja suala la miundombinu ya klabu, usajili pamoja na malengo yao, ambayo ni tofauti na baadhi ya timu za Ligi Kuu ambazo zinahubiri kucheza nne bora, lakini ukweli ni kwamba zinachotaka ni kusalia tu kwenye ligi na si vinginevyo, hivyo inatarajiwa pia msimu ujao kuwa moja ya timu zitakazomaliza ndani ya nne bora na kucheza kimataifa.
2# Simba
Itakuwa ni maajabu makubwa kwenye soka la Tanzania kama Simba isipomaliza ndani ya nne bora. Msimu uliopita ilipomaliza nafasi ya tatu na kutafsiriwa kwamba ni kufeli kwa kiwango cha juu kwa viongozi, wanachama na mashabiki wake.
Ndiyo maana ilifumua asilimia kubwa ya kikosi chake na kutengeneza kingine kipya. Nia si kumaliza ndani ya nne, bali ni kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara.
Simba ni timu ambayo ligi ikianza si kwamba inataka kumaliza ndani ya nne bora, bali kutwaa ubingwa, nafasi zilizobaki chini yake zote kwake ni kufeli.
1# Yanga
Haina mjadala kuwa Yanga itacheza mechi za kimataifa msimu ujao, hata kama isipotwaa ubingwa. Kwa sababu itakuwa ndani ya nne bora. Yanga na Simba ni timu ambazo zinaamini kuwa ubingwa umeumbwa kwa ajili yao.
Kwa sababu ni timu moja itakayoupata, basi nyingine huwa haipo mbali sana na hapo. Kama si ya pili, basi itakuwa ya tatu.
Haishangazi kuona kuwa ndiyo timu iliyotwaa ubingwa mara nyingi zaidi kuliko timu zingine, na huwa zinapokezana tu na Simba.
Yanga iliyotwaa ubingwa mara 30, na bingwa mtetezi, ndiyo timu iliyoiwakilisha Tanzania mara nyingi zaidi mechi za kimataifa, ingawa mafanikio yake huko si makubwa sana kama ilivyo kwa Simba.