Mdau wa michezo nchini aliye pia Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, amefunguka kwa mara ya kwanza sakata la kiungo Yusuf Kagoma, anayedaiwa kusaini Yanga na baadae kujiunga na Simba.
Mwigulu ametumia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram kulifafanua sakata la kiungo huyo akiandika: Sakata la Kagoma bado lipo TFF.
Nafahamu undani wa suala la Yusuf Kagoma, ni kweli Kagoma alisaini mkataba Yanga, na baadae akasaini Simba.
Najua kutokwenda kwake Yanga na badala yake kusaini Simba, hata sio masuala ya fedha. Tutatumia muda sana tukitaka kuchimba haya.
Kagoma ni mtoto wetu, Yanga ni klabu kubwa sana na ina mambo muhimu ya kuyawekea nguvu kuyafanikisha kuliko kuweka nguvu kwa Kagoma asicheze licha ya ukweli kwamba alistahili kuichezea Yanga.
NIMEWAOMBA VIONGOZI WA YANGA WASAMEHE YOTE, WAONDOE SHAURI DHIDI YA KAGOMA, WAMWACHE AWE HURU AKAITUMIKIE SIMBA KWA MASLAHI MAPANA YA MPIRA WA TANZANIA NA KWA FAIDA YA MCHEZAJI MWENYEWE.
“MY GAME IS A FAIR PLAY”
Yanga imemburuza Kagoma TFF ikidai alisaini kabla ya kuibukia Simba na kuenda kambi ya pre season ya timu iliyokuwa Ismailia, Misri.
Shauri la Kagoma, lilisikilizwa na Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji sambamba na lile la KMC dhidi ya Simba juu ya kiungo, Awesu Awesu na Geita Gold iliyokuwa ikipinga usajili wa Valentino Mashaka ndani ya Simba ambao kesi zao ilishaisha na kuanza kutumika Msimbazi.