Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mambo yametibuka…. Filamu ya Kibu na Simba iko hivi

Kibu  Simba Kauli Mambo yametibuka…. Filamu ya Kibu na Simba iko hivi

Thu, 25 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Sakata la kiungo mshambuliaji wa Simba, Kibu Denis aliyezua utata baada ya kudaiwa kutimkia nchini kimyakimya kwenda Norway ni kama filamu flani hivi kwa namna alivyowapiga chenga mabosi wake waliomtaka kuwahi kambini Misri ilipo timu hiyo ikijiandaa na msimu mpya.

Hata hivyo, taarifa zinasema kilichofanywa na Kibu kilikuwa kikifahamika kwa baadhi ya viongozi ila wamezuga ili kutowapa presha mashabiki hadi kwanza dili la Ulaya litakapotiki na kama atakwama kucheza atarudi kuendelea na timu.

Awali Mwanaspoti liliwahabarisha nyota huyo alikuwa akila bata Marekani wakati wenzake wakiwa kambini kisha ikaelezwa ishu ilikuwa pasipoti na angeondoka na kundi la mwisho la wachezaji, lakini hakuibukia na badala yake wiki hii alikwea pipa kwenda Norway, huku pande zote mbili zikishindwa kunyoosha maelezo nini kilichosababisha sintofahamu hiyo. Hata hivyo, Mwanaspoti limepata mkanda wa sakata hilo na namna Kibu alivyowatoroka mabosi wa Simba waliokuwa wakimsikilizia Dar es Salaam ili awahi kambi, wakati meneja wake akiibuka na kudai hajui kilichokuwa kinaendelea hadi alipomuona jamaa keshasepa zake Ulaya.

Kibu aliyetua Simba miaka mitatu iliyopita akitokea Mbeya City na msimu wa kwanza alifunga mabao manane, wa pili mawili na uliopita moja, na mkataba ukamalizika fasta mabosi wanamuongezea baada ya kushtuka Yanga ilikuwa ikimtolea macho na filamu nzima ilianzia hapo. Simba iliamua kumpa mkataba wa miaka miwili na nyota huyo kukunja zaidi ya Sh300 milioni akilipwa kila alichokuwa akikitaka na ligi ilikuwa imeshaisha na timu ya taifa ilikuwa na mechi za kuwania fainali za Kombe la Dunia 2026 lakini yeye alichomoa kwenda nayo kwa madai amechoka na anahitaji kupumzika.

Baadaye Kibu alionekana Marekani akila bata na familia katika maeneo tofauti ikiwemo fukwe maarufu za Miami mjini Florida, wakati tayari kambi ikiwa imeshaanza Misri na ikaelezwa awali alishatimba kabla ya Mwanaspoti kujiridhisha kulikuwa kunafichwa jambo na jamaa hakuwepo kabisa huko.

Baada ya kushtukiwa, Simba kupitia mmoja wa viongozi ilisema Kibu alikuwa akiendelea kujiuguza majeraha na muda wowote angejiunga na timu, lakini mambo yakawa kinyume baada ya kuja nchini na kufanya mchakato wa kwenda Norway alikopata mwaliko wa klabu moja ya huko.

Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally alisema alivyompigia simu Kibu ili kujua nini kifanyike kwa maandalizi ya kujiunga na wenzake, mchezaji huyo alijibu yupo Kigoma na hati yake ya kusafiria ameiacha Dar na baada ya hapo akapotea hewani.

CHENGA YA MWILI

Hata hivyo, Kibu alikacha safari ya Misri kisha baadaye kudai hati ya kusafiria imejaa na Simba kushughulikia kwa kupewa nyingine.

Licha ya kupewa hati mpya hakuwa tayari kwa safari akiwaeleza viongozi kuwa atakwenda huko atakaporejea kutoka Kigoma alikokwenda kuiona familia. Simba ikamtaka kuwasilisha hati ya kusafiria ili iandaliwe kwa kuwekwa visa ya kuingia Misri, lakini bado akaibua jipya akidai ameisahau Dar na hakuna mtu wa kuweza kuingia na wekundu hao kukwamia hapo.

ATIMKIA NORWAY

Wakati Simba ikiendelea kumsaka Kibu, ghafla zikaibuka taarifa mpya kwamba kiungo huyo ametimka kwenda Norway ikielezwa kaenda kujaribu kujiunga na timu moja inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo. Simba inaeleza ilishtuka tu kupenyezewa taarifa hizo, hata hivyo tayari mchezaji huyo alikuwa ameshatimka nchini.

Hata hivyo, habari kutoka kwa watu wa Simba ni kwamba kuna viongozi wanajua linaloendelea na walijua dili hilo mapema, na walimtafutia wenyewe na mkataba walioingia mapema utainufaisha klabu kuvuna mamilioni ya fedha, ndio maana haikuwa ajabu alikuja nchini kisha kuondoka kiulaini tofauti na inavyoelezwa ametoroka.

Inaelezwa kuwa, Simba inajifanya haijui kitu kuhofia kuingia matatani iwapo dili litatiki kwa vile klabu hiyo ni majuzi tu imempoteza Clatous Chama katika mazingira ya utatanishi aliyeenda Yanga akiungana na Jean Baleke aliyeachwa dirisha dogo lililopita huku akiwa ndiye kinara wa mabao akitimkia Libya.

“Sio kweli kama uongozi wa Simba haujui ili dili, kinachofanyika ni kuchengesha tu, ili kutowaumiza mashabiki, kwani Kibu ni mmoja wa nyota muhimu na kama wataeleza anauzwa, itawatibua,” kilisema chanzo kutoka ndani ya Simba.

Awali inaelezwa Kibu alipata ofa za Saudi Arabia na Sweden, lakini viongozi wakambania kitu kilichomzingua kabla ya kumrekebishia kwa dili la Norway na hizo taarifa eti ametoroka ni kamba za kuwazuga mashabiki, ila ukweli wanaujua.

Hata hivyo, Simba mapema juzi ilitoa taarifa iliyoonyesha kumgeuzia kibano staa huyo. Taarifa ya Simba ilisomeka: “Klabu ya Simba inautaarifu umma kuwa mchezaji wake Kibu Denis Prosper hajaripoti kambjni kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa 2024-2025.

“Tunapenda kuutarifu umma kuwa Simba tulimuongezea mkataba Kibu, Mkataba wa miaka miwili zaidi utakaoisha Juni 2026 na kumlipa stahiki zake zote za kimkataba. Hata hivyo, mchezaji huyu amekuwa akitoa sababu kadhaa wa kadha zinazomfanya kushindwa kuripoti kambini. Kutokana na utovu huu wa nidhamu klabu itamchukulia hatua stahiki za kinidhamu na umma utapewa taarifa.”

Wakati Simba ikitoa taarifa hiyo kwa umma, msimamizi na meneja wa Kibu, Carlos Sylivester alithibitisha mchezaji huyo hana madai yoyote Simba ila hakuweka wazi uamuzi wa upande wake katika sakata hili.

“Simba ilitimiza matakwa ya Kibu. Haidai timu hadi sasa lakini siwezi kuongelea mengine kwa kuwa huyo ni mchezaji wa Simba na timu hiyo inaweza kutoa maelezo zaidi,” alisema Carlos.

ASINGECHOMOKA

Kama ni kweli Kibu angekuwa ametoroka kwenda Norway ni wazi asingetoboa, kwani mkataba halali alioingia na Simba na kule kutodaiwa chochote na mchezaji huyo ilikuwa inamlazimisha kushirikisha klabu hiyo kama asingepewa mchongo huo.

Simba wakati inamuongezea mkataba Kibu ilimlipa kila stahiki ikiwemo dau la usajili na madeni ya mkataba wa nyuma kisha akakubali kuongeza wa miaka miwili.

Simba ingeweza kutumia nguvu ya kumzuia Kibu kujiunga na klabu yoyote ambapo pia hata kama majaribio hayo yatafaulu wekundu hao bado ndio wanashikilia hati yake ya uhamisho (ITC) na hapo ndio utaona ilikuwa ngumu nyota huyo kuondoka kienyeji.

Simba wanazusha sintofahamu kwani mchezaji anawezaje kujiandalia safari kwenda nje bila barua iliyotoka ndani ya klabu hiyo, hivyo kuonyesha klabu ina taarifa ya kuondoka kwake, hata kama ingekuwa kweli kuna mchezo mchafu kiungo huyo ameufanya.

MAMENEJA SASA

Pia kuna utata ulioibuka juu ya nani meneja halali wa Kibu ambapo awali wakati anaongeza mkataba alikuwa akisimamiwa na Carlos Sylvester. Baada ya kuibuka sakata la kwenda Norway akaibuka meneja mwingine aliyejitambulika kwa majina ya Rashid Yazidu.

Swali linalokuja Kibu anafanyanye mipango ya safari hizo bila ya hao wawili kufahamu au kuna mchezo wameizunguka Simba?

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: