Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sakata la Mauaji Nchini, Mapya Yaibuka

Mapya Pic Data Sakata la Mauaji Nchini, Mapya Yaibuka

Mon, 7 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kumwagiza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuunda kamati maalum ya kuchunguza mauaji ya aliyekuwa mfanyabiashara wa madini, mama wa mfanyabiashara huyo amesema anautaka mwili wa mwanawe aliodai unaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi.

Wakati huohuo, baba mzazi wa mkaguzi msaidizi wa polisi anayedaiwa kujinyonga akiwa mahabusu, Gaitan Mahembe alisema jana kuwa sasa ana imani ya kupatikana kwa ukweli badala ya kuangalia upande mmoja.

Rais Samia alitoa agizo juzi wilayani Magu mkoani Mwanza akiwa njiani kuelekea Musoma mkoani Mara kwenye maadhimisho ya miaka 45 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) yaliyofanyika jana.

Juzi hiyo hiyo, Waziri Mkuu, Majaliwa aliunda kamati hiyo yenye watu tisa itakayochunguza tuhuma za mauaji hayo yanayodaiwa kufanywa na askari polisi na mauaji yaliyofanyika wilayani Kilindi Mkoa wa Tanga.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kamati hiyo inajumuisha maofisa kutoka mamlaka tofauti za Serikali zikiwamo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Rais, Takukuru, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Pia, Waziri Mkuu alimuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro awasimamishe kazi maofisa wa Polisi wa Mtwara akiwamo Kamanda wa Mkoa na wale wa Kilindi ili kupisha uchunguzi wakati timu aliyoiunda ikifanya kazi yake.

Mama ataka mwili wa mwanawe

Mama mzazi wa mfanyabiashara huyo aliyeuawa, Hawa Bakari Ally, alisema anachokitaka ni mwili wa mwanawe ili akauzike kijijini kwao Ruponda Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi.

“Ningepata mwili wa mwanangu ningezika nyumbani nijue uko hapa mahala fulani. Vile vile ninachoona mimi kama ufuatiliaji wa mwanangu na Serikali ungekuwa mzuri, hili suala lisingefika hapa. Hili lisingetokea. Huu ni uzembe, wangefuatilia tangu Oktoba mwaka jana,” alisema.

Aliongeza: “Yaani hapa nakaa tu wala sielewi mwanangu anazikiwa wapi au anawekwa wapi. Nilichokiomba ni hata mwili ningeuona tu au ungekuja kwangu huku nizike.’’

Aliendelea kusema kuwa hata kifo cha mwanawe alikisikia kupitia gazeti la Mwananchi na baada ya hapo ameendelea kukosa ushirikiano wa Polisi kila anapokwenda kuulizia mwili wa mwanawe.

Mzazi wa polisi aliyejinyonga

Akizungumza na Mwananchi kwa simu juzi, baba mzazi wa mkaguzi msaidizi wa polisi Grayson Mahembe anayedaiwa kujinyonga akiwa mahabusu, Gaitan Mahembe alisema jana kuwa amefurahia maagizo ya Rais Samia kutaka iundwe kamati huru.

‘‘Hatua ya Rais nimefurahia sana, kuunda kamati hii naona itapata majibu ya moja kwa moja. Tusiangalie upande mmoja, binafsi naiheshimu taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi. Kwa sasa tunasubiri tuone hiyo kamati huru itabaini nini na ni hatua gani zitachukuliwa ndilo tunalolisubiri,” alisema Mahembe.

Kamati shirikishi

Pamoja na kupongeza hatua hiyo ya uundwaji wa kamati huru, baadhi ya wanasheria wametaka iwe shirikishi kwa mihimili mingine na hata kwa asasi za kiraia.

“Kosa kubwa kama hilo limefanywa hivyo lazima Rais ategemee watu nje ya Serikali. Mfano mzuri ni kesi ya wafanyabiashara wa Morogoro na ile ya Zombe na wengine,” alisema wakili mwandamizi nchini, Dk Rugemeleza Nshala akisisitiza kuwa kamati hiyo inaitwa huru lakini bado ni tu

Alisema wanapochukuliwa watendaji wa Serikali ni vigumu kupata uhakika, kwa kuwa ni watu walewale aliodai wanaweza kwenda kufumbia macho mambo.

“Hii kamati ilitakiwa iundwe na Rais mwenyewe sababu angekuwa na mamlaka ya kumteua jaji ambaye anaaminika, sasa Waziri Mkuu anamteuaje jaji? Angemteua mtu wa mhimili mwingine anayeaminika au majaji wastaafu ambao wanaaminika wawe wenyeviti, mashaka bado yapo na hata hiyo kamati imechelewa kuteuliwa. Kumekuwa na kujivutavuta miguu mpaka watu waseme huenda isiwe dhamira ya dhati pia,” alisema Nshala.

Kwa upande wake, Mratibu wa kitaifa wa mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa, alisema:

“Waziri Mkuu ameunda kamati, pamoja na kwamba haijahusisha wajumbe kutoka nje ya Serikali, bado tuna imani kamati hii itatenda haki kwa makundi yote yanayoguswa na mauaji haya kama ilivyokuwa kwa kamati za miaka ya nyuma,” alisema Olengurumwa.

Hata hivyo, Wakili maarufu nchini, Dk Onesmo Kyauke alisema hiyo ni hatua nzuri kwa sababu hata kesi ya Zombe ilipoundwa tume kuchunguza, ndipo yakabainika mengi zaidi kwa kuwa yeye alikua RPC isingekuwa rahisi kubaini ukweli.

Alisema kwa sababu kamati hiyo haitakuwa na upande wowote. Alisema huenda kamati iliyoundwa na polisi isingeleta majibu sahihi kwa sababu ilikuwa na polisi watupu, hivyo ikiwa kuna polisi wakubwa ambao wamehusika ni ngumu kuupata ukweli.

“Katika hali ya kawaida nyani hawezi kuchunguza wizi au ulaji wa mahindi shambani. Ni hatua nzuri wanachunguzwa na chombo ambacho hakina upande, ni rahisi kupata taarifa yenye ukweli zaidi kuliko Jeshi la Polisi ambalo linaweza kuwa na upande,” alisema Wakili Kyauke.

Watetezi wa haki

Kwa upande mwingine, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), jana ulitoa pongezi kwa Rais Samia kwa kutoa maagizo ya kuundwa kamati maalumu ya kuchunguza mauaji ya mfanyabiashara wa mkoani Mtwara na mauaji yalitokea Kilindi Tanga.

Mratibu wa mtandao huo, Onesmo Olengurumwa alisema uamuzi huo unadhihirisha kwa vitendo dhamira ya Rais kulinda haki za Watanzania wa kada zote.

“Kuundwa kwa kamati hiyo kumekuja baada ya kuwepo na malalamiko makubwa kutoka kwa wananchi na watetezi wa haki za binadamu kutaka tume huru iundwe ili uchunguzi huo ufanyike kwa uhuru.

Alisema THRDC inamshauri Rais Samia kuanzisha tume maalum na ya kudumu itakayohusika na kufuatilia na kufanya uchunguzi kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu katika idara za Serikali na vyombo vya usalama.

“Uwepo wa tume hii ya kudumu utasaidia kutoa haki katika tuhuma wananchi wanazoelekeza kwa vyombo vya usalama. Misingi ya utoaji haki hukataza mtuhumiwa asiwe mchunguzi wa shauri linalomhusu,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: