Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais Samia atetea tengua tengua

RAIS SAMIA KILIMO Rais Samia Suluhu Hassan

Tue, 18 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais Samia Suluhu Hassan ametetea hatua yake ya kutengua viongozi mbalimbali wa Serikali mara kwa mara, akisema uamuzi huo unafanywa kwa lengo la kulinyoosha Taifa.

Hivyo, amewataka ndugu na jamaa wa viongozi wanaotenguliwa, waache kulalamikia uamuzi wa mamlaka za uteuzi, badala yake wastahimili kinachofanyika.

Rais Samia alitoa kauli hiyo jana kutokana na mada iliyotolewa na Sheikh Sayyid Ayzuddin kutoka Kenya, aliyesema mafanikio ya Mtume Mohammad yalitokana na hatua yake ya kuwapa nafasi katika nyanja mbalimbali wale wanaostahili na si rafiki zake.

Tangu alipoapishwa kuwa Rais wa Tanzania, Machi 19, 2021, Rais Samia ametengua viongozi mbalimbali na mara ya mwisho ni Julai 3, mwaka huu alipomtengua aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mwanahamisi Athumani na Wilaya ya Kilindi, Abel Busalama.

Akizungumza katika kongamano la wanawake wa Kiislamu kuelekea maadhimisho ya mwaka mpya wa Kiislamu 1445 Hijiria, alieleza kinachoangaliwa katika uteuzi na utenguzi ni kiongozi atakayefanya vizuri na asiyefanya, lakini kumekuwa na kelele nyingi wanapowaondoa wasiofanya vizuri.

“Tustahimili kuumia kwa mwanao kuondoka, mdogo wako kuondoshwa, tustahimili kuumia ili Taifa linyooke, vinginevyo tunyooshane tangu nyumbani.

“Asifanye uzembe akaacha kazi akaenda vijiweni, sisi wakubwa huwa hatustahimili hayo, tuna mambo makubwa tumetoa ahadi ndani na kimataifa, tunataka wasaidizi wetu hawa watusaidie,” alisema.

Alisema anapoonekana mwenye uwezo wa kufanya vema kuliko aliyepo, mamlaka za uteuzi hufanya hivyo na hiyo isichukuliwe kuwa ni upendeleo.

Katika hatua nyingine, Rais Samia aliwataka wanawake kujitathmini kwa kuangalia uwezo wao katika mapambano dhidi ya changamoto ya mmomonyoko wa maadili.

Ili kufanikiwa kwenye mapambano hayo, aliwataka kwanza kujua ilipo nguvu yao, udhaifu wao na hayo wayafanye wakiwa wenyewe.

“Katika kurekebisha maadili yaliyomomonyoka, tuangalie fursa zetu ni zipi, tunaweza kufanya nini, fursa ya kwanza walimu wazuri tunao, Serikali inatuunga mkono, wengi wanajitokeza kutoa mihadhara kuwawezesha wengine,” alisema.

Alisema eneo lingine wanalopaswa kujua ni vikwazo vya kuyafikia hayo wanayoyatarajia.

“Unakuta wifi yako ana kazi nzuri anatoka anakwenda kufanya kazi, unakwenda kwake ulipomkuta unasema mwanamke gani hatulii nyumbani, hivi ndivyo vikwazo vyenyewe,” alisema.

Baada ya kuangalia hatua zote, Rais Samia alisema wanapaswa kurudi kwa Serikali kuieleza eneo wanaloweza kufanya, ili kurekebisha mmomonyoko wa maadili.

Hata hivyo, mkuu huyo wa nchi alitaka Watanzania kulinda amani, akisema ndiyo msingi wa maendeleo na uchumi wa Taifa lolote duniani.

“Juzi nilikuwa namsikiliza Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji akawa anaeleza Mei na Juni ndiyo miezi aliyopokea miradi mingi ya uwekezaji, ametaja na gharama zake.

“Lakini hayo yametokea kwa sababu kwa jirani panawaka moto, sisi kwetu kuna amani, mwekezaji hawezi kwenda eneo akiambiwa kuna fujo,” alisema.

Katika kudumisha amani, alisema ni vema watu wanapokwazana kufikia hatua ya kusuluhisha, badala ya kuishia kukwazana na hatimaye kuhatarisha amani.

Akizungumza katika kongamano hilo, Sheikh Ayzuddin alimuomba Rais Samia kutuma tume maalumu kwa ajili ya kukwamua vikwazo vya usafiri katika mpaka wa Horohoro na Lungalunga kutoka Kenya kuingia Tanzania.

“Tunasikia ushirikiano, ushirikiano lakini wallahi mtu bora upate safari ya kutoka Mombasa kwenda Canada kuliko upate safari ya kutoka Mombasa kwenda Tanga,” alisema.

Alieleza safari ya kutoka Kenya kuja Tanzania katika mipaka hiyo kuna unyanyasaji mwingi na vikwazo kwa wasafiri na hata wafanyabiashara.

“Kila ninapopata safari ya kuja nchini Tanzania mara zote naomba dua,” alisema.

Kuhusu hilo, Rais Samia alijibu atalishughulikia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: