Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais Samia ang’aka kuletewa madai yenye miaka 20

Uamuzi Wa Rais Samia Wawakosha Wakazi Wa Nanyamba.jpeg Rais Samia Suluhu Hassan.

Thu, 21 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais Samia Suluhu Hassan amesema inashangaza anapoombwa kushughulikia matatizo ya wananchi ya miaka 20 iliyopita ilhali walikuwapo viongozi waliopaswa kuyashughulikia.

Samia alisema hayo baada ya Mbunge wa Kilwa Kusini, Ally Kasinge, kumwomba aweke msukumo ili wananchi 438 wa Kilwa Masoko waliopisha ujenzi wa uwanja wa ndege tangu mwaka 2013 walipwe fidia zao.

Rais pia alikemea baadhi ya viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa wanaotumia fedha za miradi ya maendeleo kwa manufaa binafsi na kuwataka wajitathmini kama fedha zinatololewa na serikali hazitabadilisha halmashauri hiyo kiuchumi.

Alisema hayo katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika ujenzi wa bandari ya uvuvi na ugawaji wa boti za kisasa kwa wavuvi wa Kilwa Masoko, wilayani Kilwa ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake mkoani Lindi.

Katika ziara hiyo, Rais pia aliweka mawe ya msingi katika Shule ya Wasichana ya Lindi iliyoko kijiji cha Kilangala, Wilaya ya Lindi na Hospitali ya Rufani ya Mkoa katika kijiji cha Mitwero wilayani Lindi.

Alisema wakati anaingia bungeni mwaka 2010, aliyekuwa Mbunge wa Kilwa Kusini, Suleiman Buranga, maarufu kama Bwege, alikuwa akiyazungumzia madai hayo lakini anashangaa mpaka sasa hayajalipwa.

“Miaka 20 yote Kilwa si mlikuwa na viongozi? Si mlikuwa na wabunge wanawawakilisha? Kwa nini madai haya yamekaa muda wote huo bila kushughulikiwa?” Alihoji Rais Samia huku akiwataka viongozi wa halmashauri hiyo kuyaangalia tena kabla ya kumpelekea, ili wachunguze kama kuna kasoro au sababu zilizofanya kutofanyiwa kazi muda wote huo.

Pia alisema amepata taarifa za baadhi ya viongozi wakiwamo madiwani na wenyeviti wa halmashauri kuhusu usimamizi usiofaa wa fedha za miradi ya maendeleo zinazopelekwa katika halmashauri hiyo.

Rais aliwaonya wavuvi wa wilaya hiyo wanaotumia baruti katika shughuli zao kuwa zinachangia kwa kiasi kikubwa kuwapo uhaba wa samaki kwa kuwa wanakimbia kwenye maji mengi kutafuta makazi ambayo yameharibiwa.

Alisema serikali inajitahidi kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika wilaya hiyo, hivyo kama haitabadilika kimaendeleo miaka ijayo, viongozi wanapaswa kujitathmini.

“Niwaambie tu kwamba hizi fedha zinaletwa kwa ajili ya kuondoa dhiki na changamoto za wananchi. Hizi fedha haziletwi viongozi mjinufaishe. Ndio maana nasema kwa mtiririko huu wa fedha, Kilwa yetu hii isipobadilika viongozi kaeni mjitizame kuna nini ndani yenu,” alisema.

Rais alisema serikali imetoa boti kwa wavuvi na wakulima wa mwani kwa bei nafuu ikitambua hali halisi za vipato vyao na kuwasihi waliopewa zana hizo wazitumie kujiinua kiuchumi na kulipa mikopo ili itumike kununua zingine.

Pia alisema serikali ina mpango wa kujenga bandari nyingine ya uvuvi Bagamoyo ili kukidhi mahitaji ya meli nyingi zinazotarajiwa kuingia nchini kufuata fursa za uvuvi.

Kuhusu ombi lililotolewa na Kasinge kufuta hati ya eneo la mwekezaji wa Kilwa Yatch Club, Pwani ya Jimbiza, Rais alisema uamuzi huo utasababisha serikali kuilipa fedha nyingi kampuni hiyo iwapo itafungua kesi mahakamani, hivyo kuwaathiri wavuvi wanaotumia eneo hilo kujitafutia kipato.

Rais alisema matumizi ya baruti katika uvuvi yamewafanya wavuvi kufuata samaki katika kina kirefu cha maji kwa kuwa wamekimbilia huko baada ya makazi yao kuharibiwa na baruti. Aliwataka viongozi wanaosimamia sekta hiyo mkoani Lindi kusimamia suala hilo ingawa anahisi nao wanahusika katika vitendo hivyo haramu.

MAENDELEO DUNI

Akiwa katika Kijiji cha Mitwero, Rais alisema kiwango cha maendeleo katika mkoa huo ni duni kulinganisha na fursa zinazopatika yakiwano madini ya aina mbalimbali, bahari na misitu.

Aliwasisitiza wakazi wa mkoa huo kuongeza nguvu katika uzalishaji hasa katika uvuvi na kilimo cha mwani na serikali imeanza kusambaza vitendea kazi vya kisasa ili kuongeza kiwango cha mazao ya baharini.

Rais aliitaka Wizara ya Madini kuhamasisha vijana kushiriki katika uchimbaji wa madini kwa kuwa haoni sababu ya kundi hilo kutokuwa na ajira kwa rasilimali za kutosha zinapatikana mkoani humo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, alisema ujenzi bandari hiyo uliogharibu Sh. bilioni 280, unaonyesha nia na dhamira ya dhati ya Rais ya kuinua sekta ya uvuvi nchini.

Alisema ujenzi huo utaongeza fursa za kiuchumi wa Kilwa na kanda ya kusini kupitia uwekezaji na kuongeza mchango wa sekta kwa taifa kutoka asilimia 1.8 ya sasa hadi 10 ifikapo mwaka 2036.

Ulega pia alisema bandari hiyo itakuwa na karakana ya kutengeneza meli na nyavu za kuvulia samaki, hivyo kuondoa gharama za kuagiza nje ya nchi.

Pia alisema bandari hiyo uwezo wa kupokea meli 10 zenye ukubwa wa mita 30, eneo la kuhifadhi samaki tani 90 walioganda na walioyeyuka tani 1,300 kwa wakati mmoja hivyo kutoa ajira kwa vijana takribani 30,000.

Alisema boti 160 zinazotolewa kwa wavuvi na wanawake zitawawezesha kuvua samaki na kulima zao la mwani kwenye maji ya kina kirefu na kuondoa changamoto waliyokuwa nayo muda mrefu na kurudisha nyuma juhudi za kuletea maendeleo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: