Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais Samia aanika madudu haya kwa viongozi

Wakipotosha, Toeni Majibu Haraka Rais Samia Rais Samia Suluhu

Fri, 3 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais Samia Suluhu Hassan, amesema pamoja na Tanzania kupiga hatua kwenye siasa safi, kuwa na ardhi ya kutosha na watu lakini kuna shida kwenye uongozi bora.

Aliyasema hayo jana jijini hapo wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha viongozi wa serikali wakiwamo mawaziri, manaibu wazari, makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu.

“Ndugu washiriki karibuni sana kwenye kikao kazi ambacho lengo kuu ni kukumbushana na kueleweshana juu ya kutimiza ipasavyo wajibu tulionao na dhamana tuliyoibeba ya kuwatumikia wananchi.

“Baba wa Taifa (Julius Nyerere) aliwahi kutueleza kuwa ili taifa letu liendelee tunahitaji mambo manne nayo ni watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.

“Mtakubaliana nami watu tunao wa kutosha idadi yetu ni milioni 67, ardhi tunayo tena kubwa ingawa tuna migogoro kadhaa, siasa safi na yenyewe ipo kwasababu tunapotoka nje ya nchi sifa tunazopata ni kutokana na siasa safi tuliyonayo.

“Suala hapa lenye shida labda ni uongozi bora sasa hili tutakwenda kuliangalia hapa na kulijadili, tujifunze mambo yanayomfanya kiongozi awe bora ili tuisaidie nchi yetu.”

MIGOGORO

Alisema kutokufanyika vikao kazi kwa muda mrefu kumesababisha athari serikalini zinazoonekana wazi katika utendaji kazi wa viongozi wa wizara mbalimbali na kuwapo kwa ombwe la uelewa wa utaratibu wa utendaji kazi serikalini.

Alisema hali hiyo inasababisha migongano isiyokuwa ya lazima kwa viongozi hao na kuathiri utendaji kazi na uwezo wa kuwahudumia wananchi.

Vilevile, alisema sababu hiyo imechangia viongozi kubadilishwa mara kwa mara, ili kuepusha serikali na fedheha ya kuwa na viongozi wanaoifanya wizara kuwa sehemu ya malumbano na migawanyiko isiyokuwa na tija.

“Ninafahamu madhara ya kubadilisha viongozi mara kwa mara na sipendi kufanya hivyo kwa sababu kunafanya watu wafanye kazi kwa hofu na viongozi wasiwe na mipango ya muda mrefu kwa kuhofia teuzi zao kutenguliwa,” alisema Rais Samia.

Alifafanua kuwa kiongozi anapotolewa kazini ni fedheha kwa familia yake, watoto na vijiana ambao walikuwa wakimwona kama mtu wa mfano kwao.

“Mimi sio lengo langu kubadilisha viongozi mara kwa mara kwa kuwa huchukua muda mrefu kuwajenga hata na wakati mwingine ninalazimika kufanya hivyo ili kuepusha madhara kutokea zaidi serikalini na kwa wananchi.”

Matumaini yake ni kuwa mkutano huo, utawaongezea ujuzi katika uongozi na utasaidia kuboresha utendaji kazi, kuondoa migongano na kuleta ufanisi na tija katika kutoa huduma kwa wananchi.

“Viongozi wazoefu ndio wanafanya viongozi wapya kuwaiga wakijua kwamba kuwa na migogoro, kutokufuata sheria utaratibu ni jambo la kawaida serikalini.

Kadhalika, Rais Samia alisisitiza suala mgawanyo wa majukumu, mipaka ya madaraka kwa viongozi hao, dhana ya uongozi na sifa ya kuwa kiongozi bora.

“Nimekuwa nikisisitiza kila wakati nyinyi kwa pamoja ni timu moja ya uongozi na utawala katika wizara kama viongozi mnategemewa kuonyesha njia kubuni nini kifanyike katika kutekeleza majukumu ya wizara mlizokabidhiwa kuziongoza kwa kufuata sheria, kanuni, miongozo na utaratibu wa serikali tuliojiwekea.”

Aliwakumbusha viongozi jukumu la utawala wanategemewa kuwa makini na mahiri katika kusimamia kutumia rasilimali watu, vifaa na fedha za umma, pamoja na kuwa na mipango na mikakati thabiti ya kutekeleza na kusimamia majukumu hayo.

“Ili muweze kutimiza kwa ukamilifu wajibu wenu hamna budi kutambua vyema mipaka yenu ya uongozi na mamlaka na njia nzuri ya kuyajua haya ni kwa kusoma miongozo ambayo wanapatiwa baada ya kuteuliwa na kula kiapo,” alisema.

MAOFISA HABARI BINAFSI

Aliwataka viongozi wa serikali kusemea mambo mazuri na mafanikio yaliyofikiwa na serikali badala ya kutoa nafasi kwa baadhi ya watu wasiokuwa na nia njema kufanya upotoshaji.

“Viongozi tumekuwa wazito kusemea mafanikio mengi tunayoyapata hivyo kuacha watu wengine kuendelea kufanya upotoshaji na kuna msemo unaosema uongo ukisemwa mara nyingi unageuka kuwa ukweli.”

Amesema serikali imefanya mambo makubwa yaliyosaidia kutatua shida na kero za wananchi na kwamba ni wajibu kwa viongozi hao kutoa taarifa jinsi serikali ilivyotatua shida hizo.

“Nimewahi kuona kiongozi mmoja wa kisiasa akiilaumu serikali kwamba inatumia fedha nyingi kutafuta vyanzo vipya vya maji kupeleka kwa wananchi, lakini kuna visima kadhaa vilichimbwa nyuma na vimeachwa na tunatumia fedha nyingi kupeleka maji kwa wananchi.

“Ni kiongozi huyu huyu ambaye kuna kipindi yeye mwenyewe alisema kwa mfano hapa Arusha kulichimbwa visima vingi, lakini maji yote yalikuwa na chumvi hayakufaa kutumika kwa matumizi ya binadamu.

“Sasa kiongozi huyu huyu anasema serikali imeviacha visima na tumekwenda kutumia pesa nyingi kutafuta vyanzo vingine na kupeleka maji kwa wananchi.”

Alisema wizara inayohusika na jambo hilo ilitakiwa kujitokeza haraka kutoa majibu yenye ukweli, takwimu halisi na kumweleza mhusika kwa nini visima hivyo vimeachwa au havikuachwa.

“Nakumbuka wakati wa shida ya maji Mkoa wa Dar es Salaam ni visima hivi hivi ambavyo viliwekwa akiba viliwafaa wananchi, sasa mambo kama hayo kuweni wepesi wa kutoa majibu mnapomsikia mtu anapotosha na huu ni mfano mmoja, lakini iko mingi ya aina hii hivyo muwe wepesi wa wizara zenu kutoa taarifa.

“Najua kila wizara ina vitengo vya habari, je vinatumikaje au viko tu vimekaa havifanyi kazi, lakini bado baadhi ya mawaziri mmeajiri maofisa wenu wa habari binafsi wa kutoa taarifa zenu na sio za serikali, sasa mambo kama haya twendeni tukarekebishe na nimatumaini yangu kuwa mada kuhusu suala hili itatukumbusha wajibu wetu kama viongozi na wasemaji wakuu wa wizara zetu,” alisema.

Alisema utoaji wa taarifa unapaswa kuzingatia kanuni na utaratibu, ili kuepuka kutoa taarifa zinazokinzana ndani ya taasisi moja na serikali moja.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: