Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais Samia: Nilibezwa sasa!

Samia Road.jpeg Rais Samia Suluhu

Mon, 20 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais Samia Suluhu Hassan, amesema pamoja na mafanikio yanayoonekana sasa nchini, anakumbuka namna alivyoingia madarakani kwa kubezwa kutokana na dhana miongoni mwa jamii kuhusu jinsia ya kike, kwamba inaweza kufanya kazi ipasavyo na kuleta mabadiliko.

Aidha, amesema kwa kipindi cha miaka miwili, kipekee anawashukuru wanaume ambao nao wamefanikisha hatua za kimaendeleo zilizopigwa nchini, kipindi ambacho amefanya kazi nzuri na kubwa na tafsiri hiyo inajionyesha wazi.

Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, kwenye sherehe ya kumpongeza kutimiza miaka miwili tangu aingie madarakani Machi 19, mwaka 2021 zilizoandaliwa na Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT).

Kadhalika, sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi na wanachama wa Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA), zilizofanyika Uwanja wa Uhuru, jijini humo.

Katika hotuba yake ilichukua takribani dakika 40, Rais Samia alijikita zaidi kuzungumzia mafanikio, changamoto zinazomkabili mwanamke wa Kitanzania, akisisitiza kwamba mwanamke anapopewa nafasi na kupewa nguvu anaweza.

“Tulipoanza mwaka 2021 bezo lilikuwa kubwa, lakini bezo…unapobezwa unajenga ujasiri na kazi inaendelea. Nawashukuru wanawake kwa kunipa nguvu, nguvu kwa kuwa nimeweza. Pongezi hizi ziende kwa wanawake Watanzania wote,” alisema Rais Samia.

MIRADI KIMKAKATI

Alisema, wakati anaingia madarakani aliikuta miradi ya kimkakati iliyoanzishwa na mtangulizi wake, Hayati John Magufuli, ikiwamo ya ujenzi wa reli ya kisasa na barabara na ambayo amehakikisha inaendelea kutekelezwa ipasavyo, ili kuifungua kiuchumi nchi barani Afrika na duniani.

“Niliahidi kuzitekeleza kazi za mwenzangu na mpaka sasa hakuna kilichosimama, kwa pamoja tumshukuru Mungu. Lengo la kuanzisha Wizara ya Jamii, ni kumsogeza mwanamke kutoka aliko na kupunguza unyanyaji wa wanawake na watoto,” alisisitiza Rais Samia.

Alisema katika kipindi cha miaka miwili hazikukosekana changamoto hasa zikichangiwa na mambo kadhaa kama vile vita nchini Ukraine, Uviko-19 pamoja na mabadiliko ya tabianchi, ambayo yanasababisha chakula kisizalishwe kwa wakati.

“Changamoto hizi zinasababisha bei za chakula zipande, adimu, niwahakikishie wananchi kama tulivyofanya kwenye mafuta (petroli/dizeli) na kuweka ruzuku ya Sh. bilioni 100, ili bei ziwe za wastani, ndivyo tumechukua hatua sekta nyingine,” alisema Rais Samia na kuongeza:

“Hata katika mbolea, tulitoa ruzuku na serikali ilichukua hatua kupunguza makali ya uchumi, ili Watanzania kuwa na ustawi mzuri. Mkutano wa mapinduzi ya kijani katika ukanda wa Afrika Mashariki unatisha, ila Tanzania bado tuko vizuri. Fedha za kigeni, Tanzania bado iko vizuri.’

“Ndugu zangu kuna changamoto kubwa moja ambayo huwa hatuizungumzii, tunasema ajenda ya wanawake ni moja, lakini tunapokuwa kwenye siasa tunagawanyika. Sisemi wote tuwe na itikadi moja…yanayomsibu mwanamke wa Kitanzania lazima tuyasemee.

“Manyanyaso yanayotokea kwenye siasa vyama, lazima tuseme, tubadilike, tunaposimama majimboni tuungwe mkono na si kusimamishwa kimtego mtego, kwa ambayo yanayotuhusu tusimame pamoja.”

KATIBA MPYA

Kuhusu Katiba mpya, Rais Samia alisema nia ipo, ndiyo maana akafungua milango ya mazungumzo ikiwamo maridhiano, akiamini kila japo linakwenda kwa hatua.

“Tumesema Katiba mpya, tunataka ibadilike tumesema sawa, kila jambo ni kwa hatua kwa hatua, sifa ya Tanzania ambayo tumeijenga kwa utawala bora lazima tuijenge. Mimi kama mwanamke najiamini, sifa ya mwanamke ni kujiamni, nimefungua uwanja wa siasa, CCM nikiamini tuko pamoja na tutajadiliana kwa pamoja,” alisema.

Aidha, katika kumkwamua mwanamke na vikwazo vya kiuchumi, kwenye sekta mbalimbali, alisema serikali yake ilipounda Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, lengo ni kuiinua jinsia hiyo.

“Wanawake ni wajasiriamali wanaouza bidhaa mbalimbali ndani na nje ya nchi. Tanzania ni lazima tuwe mabingwa kusimamia mwanamke kukuzwa kiuchumi, lazima nionyeshe kivitendo, ndani ya nchi yangu nasimamia mwanamke kukuzwa kiuchumi.”

“Tunataka masoko ambayo yanaweza kumfanya (mwanamke) akafanya shughuli zake na kumlea mtoto wake. Nataka kuonyesha kwa vitendo,” alisema Rais Samia.

USAWA 50/50

Kadhalika, alisema ili kufikia lengo la 50/50 kwenye nafasi ya mwanamke katika uongozi, kuna ongezeko la nafasi za wanawake kiuongozi akitaja Mahakama Kuu ina majaji 86 kati yao 40 ni wanawake na maofisa tawala wa mikoa 26 kati yao 12 ni jinsia hiyo huku bungeni akisema bado kuna kazi ya kufanya.

“Bungeni nako tunakwenda polepole kama sio 50 basi asilimia 40 tujitokeze kwa wingi kwenye uchaguzi. Wanawake ajenda yetu ni moja, sasa tutakwenda kwa awamu mwaka huu wameanza BAWACHA (Baraza la Wanawake wa Chadema) kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, mwaka kesho ACT-Wazalendo.”

Alisema serikali yake imejikita kumkwamua Mtanzania kiuchumi, kutokana na Ilani ya CCM, akisema kaulimbiu ya mwaka huu ya siku ya Wanawake Duniani; Teknolojia na Ubunifu ndio msingi wa maendeleo, iwe msingi wa maendeleo.

“Hatujayamaliza yapo yanayokosesha huduma wanawake, lakini katika elimu tunakwenda kujenga shule za sayansi kwa wasichana kwenye kila mikoa na VETA (Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi), kila wilaya, ili wawe wabunifu.”

Kuhusu sekta ya afya, Rais Samia alisema maboresho yanaendelea na kuhusu mfumo wa M-MAMA unaolenga kunusuru vifo vya wanawake wanaojifungua tayari umeokoa maisha ya mama na mtoto.

Vilevile, katika sekta ya kilimo, Rais Samia alisema kutokana na kilimo kuajiri zaidi vijana, serikali yake imeanzisha shamba litakaloahusisha vijana ambalo linazinduliwa leo (Machi 20, mwaka huu) jijini Dodoma.

“Teknolojia inasaidia kuokoa muda, miundombinu bora ya anga na nchi kavu, reli, barabara inasaidia Watanzania kuchukua muda mfupi. Dar es Salaam yote imejaa vumbi, kazi inaendelea, Dodoma nako inaruka vumbi kurahisisha usafiri.

“Katika bandari pia tunajenga bandari zetu, ili kurahisisha biashara ndani ya bara la Afrika. Tuliachiwa miradi mikubwa miwili ya kimkakati na kazi inakwenda, itaongeza tija kwa shughuli za kijamii na kiuchumi,” alisema Rais.

Kadhalika, kuhusu mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na kila halmashauri nchini, takwimu inaonesha iliyokopeshwa kwa asilimia 88 fedha hazijarejeshwa hivyo kuna haja ya kufuatilia suala hilo.

Katika mkutano huo wanawake wa vyama vya upinzani vya ACT-Wazalendo na CHADEMA walihudhuria.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: