Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Olengurumwa ataka wapinzani kumwachia Samia urais 2025

Rais SAMIA KICHEKO.png Rais Samia Suluhu Hassan

Thu, 23 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa, ameshauri wapinzani kutosimamisha wagombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Amesema kwa mtazamo wake, kutokana na Rais Samia Suluhu Hassan kuonyesha nia ya majadiliano na upinzani, huku vyama vya siasa vikianza kurejea tangu kufungiwa shughuli zao kwa takribani miaka saba, ni vyema vikaacha nafasi hiyo ili kukuza utawala bora.

Olengurumwa aliyasema hayo hivi karibuni kwenye mahojiano akizungumzia miaka miwili ya Rais Samia madarakani huku akisisitiza kuwa hiyo ni hoja yake binafsi.

“Kwa mimi nataka niwashauri vyama vilivyoshindwa kufanya kazi. Tanzania tuliua upinzani, hivyo kwanza wajipange. Upinzani wawekeze kwa ajili ya uchaguzi unaokuja wa serikali za mitaa na kwa uchaguzi wa mwaka 2025 wawekeze kwenye madiwani na ubunge.

“Wafanye hivyo hivyo angalau wapate wapate theluthi ya wabunge, theluthi madiwani na wenyeviti wa vijiji. Wakifanya hivyo kwa uchaguzi unaokuja wa mwakani (serikali za mitaa) na uchaguzi mkuu mwaka 2025, hadi uchaguzi wa mwaka 2030 wataweza kusimamisha wagombea urais. Uchagzui wa 2025 ukiwa wa haki wapinzani watapata viti vya ubunge, udiwani na mitaa. Waingie makubaliano na rais katika uchaguzi huru na haki,” alisema.

Alisisitiza kuwa ili kuwa na mgombea urais ni pesa, na kwa uhalisia wapinzani pia wana tatizo hilo, hivyo wawekeze kwa wagombea udiwani na ubunge. Olengurumwa alisema kwa mtazamo Rais aliyeko madarakani anatekeleza misingi yao (wapinzani) kama vile haki ambayo imetolewa na sasa wanafanya shughuli zao za kisiasa.

“Tumuunge mkono hata kama vyama havitanufaika kisiasa sasa lakini tutakuwa tumeepusha kizazi kwa miaka ijayo kuja kuwa na siasa za chuki,” alisema.

Kuhusu mtazamo wa asasi za kiraia (AZAKI) juu ya masuala ya utawala bora nchini, alisema ukimya wa matamko unamaanisha uwapo wa kiwango cha haki za binadamu, usawa na uhuru wa vyombo vya habari.

“Rais Samia Suluhu Hassan kwa kipindi cha miaka miwili tangu aingie madarakani na kuigusa katiba hasa kwenye eneo la utawala bora na haki, sasa mifumo hiyo ilindwe kitaasisi na kisheria. Tutaonekana ni watu ambao hatujui tunachokitaka, kusimama na kuanza kupinga hakuna sababu, amerudisha demokrasia, ameshiriki mikutano na wapinzani.

“Kimsingi watetezi wa haki za binadamu tunataka tuone viongozi wetu wakiheshimu haki za binadamau, kiongozi akiwa kinyume na utawala bora utatuona sisi tukiwa mbele na matamko ya kushauri,” alisema.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa kuna haja ya kuwa na bunge bora ambalo linaweza kukosoa na kutoa mwelekeo ambao una dhamira njema kwa taifa.

“Tulifika hatua bunge lilikuwa na wabunge karibu nusu kwa nusu, mabadiliko tunayoyaona yalitokana na bunge. Kama Escrow ilitokana na mijadala ya wabunge wa pande zote,” alisema.

Pia alisema mihimili mingine pia ambayo inahitaji kuimarishwa na kiongozi wa nchi na kuwa na uhuru kwenye utendaji wao ni mahakama na vyombo vya habari ambavyo hutoa mchango mkubwa wa kuibua kero, yakiwamo masuala ya rushwa.

Ole Ngurumwa, alieleza kwamba utashi wa kisiasa aliouonesha Rais Samia, ni mwanzo wa ujenzi mpya wa siasa za kistaarabu na za kuigwa barani Afrika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: