Mwanamke mmoja mkazi wa Kijiji cha Manda Chini, Tarafa ya Mengwe, Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, Patricia Kisela (57) amejiua kwa kujinyonga na kamba ya kufungia ng'ombe, ikidaiwa sababu ni kuzidiwa na madeni ya Vikoba.
Mama huyo ambaye ni mjane, alijiua asubuhi ya Desemba Mosi, 2023 siku moja baada ya kutoka hospitali alipokuwa amelazwa baada ya kufanya jaribio la kutaka kujiua kwa kunywa sumu.
Inadaiwa kuwa, mwanamke huyo ambaye ni mfanyabiashara wa ndizi katika soko la Mamsera alikuwa akitamka maneno ya kutaka kujiua baada ya biashara yake kuzidiwa na madeni mengi kutokana na kukopa katika vikoba mbalimbali zaidi ya Sh900,000.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mwenyekiti wa kijiji cha Manda chini, Ernest Mrosso alisema tukio hilo limetokea asubuhi Desemba Mosi, mwaka huu, huku akieleza sababu kubwa ni wingi wa madeni aliyokuwa nayo.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema sababu za matukio hayo ya kujinyonga yanatokana ma msongo wa mawazo na ni suala la kifamilia zaidi.
"Kwenye kujinyonga kuna sura mbili, msongo wa mawazo lakini ni masuala ya kifamilia zaidi, akinyongwa hilo ni la kijinai, kwa hiyo suala hilo la mtu kujinyonga ni la kifamilia lakini tunafuatilia zaidi,"amesema Kamanda Maigwa.