ARUSHA: Kijana James Sindio mwenye umri wa miaka 16 anatuhumiwa kumuua kaka yake anayeitwa Zakayo Sindio huku baba mzazi akikiri kushindwa kuwaamua ndugu hao wawili waliokuwa wakigombana kisa mifugo.
Mimi naitwa Paulo Sindio, ni baba mzazi wa watoto hao, walianza kugombana mbele yangu kisa kikiwa ni uswagaji wa mifugo kurudi porini, wote ni watoto wangu na wa mama mmoja.
Akielezea tukio hilo, Paulo amesema: “Walikorofishana baada ya mkubwa kumwambia mdogo kuwa anatakiwa kwenda kuswaga mifugo kauli ambayo ilipingwa na James na baada ya muda wakaanza kupigana.
“Walipigana, mimi nikanyanyuka kwa ajili ya kwenda kuwaamua, kumbe mwenzake tayari alikuwa ameshamchoma kisu kwenye moyo, tulivyompeleka hospitali ikakutwa ameshafariki.
“Sina la kusema, wazee wa ukoo wapo wataamua wenyewe, sina la kufanya, na sijui alipo, kama ameenda kujiua au la sijui alipo. Polisi tayari wana taarifa na wanalifuatilia.”
Jeshi la Polisi mkoani Arusha limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa wanaendelea kumsaka kijana James kwa tuhuma za mauaji hayo ya kaka yake.