Mechi za kimataifa kwa timu za taifa zimemalizika juzi usiku baada ya kupigwa raundi mbili kwa kila kundi katika msako wa tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025, huku wachezaji wa Yanga walioitwa katika timu hizo wakifunika mbaya ukilinganisha na wachezaji wa timu nyingine.
Yanga ilitoa jumla ya wachezaji 14 kwenda katika timu tofauti za taifa ambazo kuanzia Septemba 2 hadi 10 zilikuwa na mechi za kuwania kufuzu ushiriki wa Afcon 2025.
Kati ya wachezaji hao 14, ni wawili tu ambao hawakupata fursa ya kuzichezea timu zao za taifa ambao ni kipa Abuutwalib Mshery wa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' na kiungo Stephane Aziz Ki wa Burkina Faso.
Lakini wengine 12 wamepata dakika za kucheza ambazo hapana shaka zmewapa ufiti na kuwaweka katika hali nzuri kimwili kwa ajili ya mechi inayofuata ya Yanga dhidi ya CBE ya Ethiopia katika raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo itachezwa Jumamosi saa 9:00 alasiri.
Katika hao 12 ambao walipata nafasi ya kutosha ya kucheza, watatu wametumika kwa dakika nyingi zaidi kwenye timu zao za taifa ambao ni Ibrahim Hamad 'Bacca' na Clement Mzize waliokuwa katika kikosi cha Taifa Stars ambao kila mmoja amecheza kwa dakika 180 ikiwa ni wastani wa dakika 90 kwa mchezo katika mechi mbili dhidi ya Ethiopia na Guinea kama ilivyo kwa Djigui Diarra ambaye timu yake ya taifa ya Mali ilicheza na Msumbiji na Eswatini.
Anayefuatia ni Khalid Aucho wa Uganda ambaye amecheza kwa dakika 178 katika michezo dhidi ya Afrika Kusini na Congo sawa na wastani wa dakika 89 kwa mechi na nyuma yake yupo Duke Abuya aliyecheza kwa dakika 176 katika mechi mbili za Kenya dhidi ya Zimbabwe na Namibia ikiwa ni wastani wa dakika 88 kwa mechi.
Kennedy Musonda ameichezea Zambia kwa dakika 165 katika mechi mbili dhidi ya Ivory Coast na Sierra Leone huku mwenzake Clatous Chama akitumika kwa dakika 155, wakati katika kikosi cha Zimbabwe, Prince Dube akicheza kwa dakika 161 dhidi ya Kenya na Cameroon.
Wachezaji wengine wa Yanga ambao walikuwa katika kikosi cha Taifa Stars na muda waliocheza kwenye mabano ni Mudathir Yahya (124), Dickson Job (101), Bakari Mwamnyeto (79) na Nickson Kibabage aliyecheza kwa dakika 46.
Mbali na kundi kubwa la wachezaji wa Yanga kupata muda wa kutosha wa kucheza, watatu kati yao wamefunga mabao yaliyotoa mchango mkubwa katika kuziwezesha timu zao za taifa kupata ushindi katika mechi za raundi ya pili.
Kennedy Musonda alifunga bao la kwanza katika ushindi wa mabao 3-2 ambao Zambia ilipata dhidi ya Sierra Leone na akatoa asisti ya bao la pili, huku Mudathir Yahya akiifungia Taifa Stars bao la pili katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Guinea kama ilivyokuwa kwa Duke Abuya aliyefunga katika ushindi wa mabao 2-1 ugenini ambao Kenya iliupata kwa Namibia.
Simba yenyewe ilikuwa na wachezaji wanne katika timu za taifa ambao watatu walikuwa katika kikosi cha Taifa Stars na mmoja katika kikosi cha Guinea.
Wachezaji waliocheza kwa dakika nyingi zaidi ni Mohammed Hussein na Ally Salim ambao kila mmoja amecheza kwa dakika 180 kwenye kikosi cha Taifa Stars sawa na wastani wa dakika 90 kwa mechi.
Katika kikosi hicho cha Taifa Stars, alikuwepo Edwin Balua pia ambaye alitumika kwa dakika 131 sawa na wastani wa dakika 65.5 kwa mechi huku kipa Moussa Camara katika kikosi cha Guinea akisotea mkeka katika mechi zote mbili ilizocheza dhidi ya DR Congo na Tanzania.