Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Familia yasimulia ndugu yao alivyopotea

RPC MAGOMI Bn Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, Janeth Magomi.

Wed, 8 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Familia ya Issa Hamis Issa (44) ambaye ni fundi magari mkazi wa Ndala Manispaa ya Shinyanga, mkoani Shinyanga imesimulia namna ndugu yao alivyopotea katika mazingira ya kutatanisha kwa takribani miezi mitatu sasa.

Issa anadaiwa kupotea miezi mitatu iliyopita akiwa na mwenzake aliyefahamika kwa jina la Perezi Bwee.

Akisimulia tukio hilo jana mdogo wake Issa, Hussein Hamis alisema ndugu yake huyo alipotea tangu Novemba mwaka jana akiwa na mwenzake (Bwee) na mpaka sasa hawajui walipo.

Alisema siku aliyopotea ndugu yake alitoka nyumbani majira ya asubuhi akiwaaga kuwa anakwenda kwenye shughuli zake za utengenezaji magari, lakini siku hiyo hadi jua linazama hakurudi nyumbani.

Alisema walipofuatilia kazini kwake wakaambiwa kuwa waliaga wanakwenda Mwanza na walipopiga simu zao zilikuwa hazipatikani.

Aliendelea kusimulia kuwa baada ya kaka yake kutopatikana kwenye simu pamoja na kumkosa kwa ndugu zake wote, walienda kutoa taarifa Kituo cha Polisi Shinyanga ili kuwasaidia kumpata, lakini mpaka sasa hakuna taarifa zozote wala hawajui aliko yeye na mwenzake.

“Baada ya kumkosa kaka yangu kwenye vituo vyote vya polisi pamoja na hospitali ili kujua huenda labda alipata ajali, ndipo ikabidi tupekue kwenye kitabu chake cha kumbukumbu (daily) na katika kupiga tukapata namba moja ikasema ndugu yetu anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mwanza,”alisema Hamisi.

Alisema walipofuatilia polisi Mwanza wakaambiwa hayupo kituoni hapo ndipo wakapiga tena ile namba wakaambiwa yupo Kituo cha Polisi Dodoma.

Akisimulia zaidi, alisema walipokwenda katika Kituo cha Polisi Dodoma wakaambiwa hayupo, ndipo wakapiga tena simu kwenye namba ile ile wakaambiwa yupo Kituo cha Polisi Dar es Salaam.

“Tulipoipigia tena ile namba tukauliza wamekamatwa kwa kosa gani? huyo mtu akatueleza kuwa wameiba gari la mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), lakini cha kushangaza huyo mtu hataki kujitambulisha yeye ni nani na akiongea kidogo anakata simu,” alisema.

Alisimulia kuwa wakarudi tena Kituo cha Polisi Shinyanga kufuatilia taarifa za ndugu yao, wakaambiwa bado hawajampata kwamba wanaendelea kumtafuta na akipatikana watapewa taarifa.

 Alisema kuwa ndugu yake ana watoto wawili, mmoja ana miaka sita na mwingine mwaka mmoja, hivyo analiomba Jeshi la Polisi liwasaidie kumtafuta kaka yake ili wajue mahali alipo.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, Janeth Magomi, alithibitisha kuwepo kwa taarifa za kupotea kwa Issa Hamis Issa na kusema bado wanaendelea kumtafuta.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: