Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baba, mtoto wauawa wakidaiwa kuua mtoto mwenye ulemavu

Baba Picds Baba, mtoto wauawa wakidaiwa kuua mtoto mwenye ulemavu

Tue, 23 Jul 2024 Chanzo: Mwananchi

Mkazi wa Kijiji cha Ilabilo Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, Stephano Ndagiwe na mtoto wake, Alfayo Stephano (14) wameuawa na wananchi wa kijiji hicho, baada ya kutuhumiwa kuhusika na mauaji ya mtoto mwenye ulemavu, Simoni Furaha (5).

Akizungumza jana Julai 21, 2024, mkuu wa wilaya hiyo, Kanali Evance Malasa amesema watu hao waliuawa baada ya mtoto Simoni, mwenye ulemavu wa miguu na mikono kupotea kwa siku mbili kuanzia Julai 18 mwaka huu na kupatikana Julai 20 akiwa amezikwa jirani na nyumba ya Ndagiwe.

“Simoni alipotea Alhamisi ya Julai 18, 2024 na mwili wake kukutwa Julai 20, 2024 ukiwa umefukiwa katika kichaka jirani na makazi ya watu kijijini hapo, huku ukiwa na ishara ya kunyongwa,” amesema.

Kanali Mlasa amesema baada ya wananchi kumpata mtoto huyo akiwa amezikwa, walimtafuta Ndagiwe na kumuua, baada ya kukimbia alipohojiwa kuhusu uhusiano wa mtoto huyo kupotea na kukutwa kafukiwa karibu na eneo lake.

Kwa mujibu wa Kanali Malasa, hadi watu sita wanashikiliwa na Jeshi la Polisi wakidaiwa kuhusika na mauaji hayo, huku miili ya marehemu wote watatu ikizikwa leo.

Akisimulia tukio hilo, baba mdogo wa marehemu Simon, Gipson Enock amesema baada ya wananchi hao kumuua baba na mtoto, walichoma moto nyumba yao na kukatakata mazao shambani, kisha kuanza kumtafuta kijana wake waliyedai alikuwa na tabia za kikatili, ikiwemo kunyonga mifugo bila woga.

Amesema kijana huyo alikutwa kwa moja ya ndugu zake na alipowaona alianza kukimbia hadi nyumbani kwao.

“Alikuta nyumba yao inaungua moto, kisha wanakijiji hao walimkamata na kumchoma moto hadi kufariki dunia wakidai wanaangamiza watu katili kijijini hapo,” amesema.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Kakonko, Maulid Mtulia amesema kutokana na baba na mtoto wake kuuawa na wananchi, hata ndugu wameogopa kufika nyumbani kwao wakihofia usalama wa maisha yao. Mke wa Ndagiwe hajulikani alipo.

Akizungumza na wananchi baada ya kufika eneo la tukio, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye amewataka kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi, badala yake watoe ushirikiano kwa vyombo vya dola, ili vifanye kazi yake ya kuwabaini watuhumiwa na kuwafikisha mahakamani.

“Hebu turudi, tushikamane, tuwe wamoja, tusaidiane kwa sababu hicho kitu ndio kitakachotusaidia.

“Pia wote kwa pamoja tushirikiane na Jeshi la Polisi na wengine wa kamati ya ulinzi na usalama kuwabaini, kuwakamata na kuwaumbua watu wote ambao wametenda uhalifu ama wamepanga kuutenda,” amesema.

Chanzo: Mwananchi
Related Articles: