Naibu Spika, Musa Zungu ameitaka klabu ya Simba kufanya usajili wa maana ila uwe wa kimya kimya.
Akizungumza juzi katika sherehe ya chakula cha usiku iliyoandaliwa na tawi la Simba Mjengoni, jijini hapa ambalo ni maalumu kwa ajili ya wabunge na wafanyakazi wa taasisi za uuma na binafsi, Zungu alisema matokeo ya msimu uliopita yaliwaumiza hivyo ni lazima wakae chini na wachezaji na kuzungumza nao.
Sherehe hizo zilihudhuriwa na mawaziri, wabunge na mashabiki wa klabu hiyo wakiongozwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Hamad Masauni, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma, Mwana FA.
“Kuna baadhi ya wachezaji wetu wapewe ushauri haiwezekani kuwa na kiwango cha kutuvunja moyo, lakini nimekaa hapo kuna mtu kanitumia meseji anasema nyie chezeni tu hapo Dodoma sisi tunasajili “Mimi niwaombe viongozi wa Simba mnafanya jambo jema kuficha usajili wenu msituambie mje mtusaprise ila msituue, mtusaprize kwa mafanikio.
“Mmetueleza mipango jambo jema na Simba tusiingie unyonge mkitazama mechi za Ligi ya Mabingwa huwezi kumlaumu kiongozi kocha wala mchezaji, haikuwa bahati yetu ni mipango ya Mungu,” alisema.
Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo,Imani Kajula alisema wamejipanga msimu ujao kufanya vizuri kwa kutenga bajeti ya Sh23 bilioni kwa ajili ya uendeshaji wa klabu hiyo.
Mtendaji huyo alisema dira ya klabu hiyo ni kuwa timu inayoongoza Afrika huku akivitaja vipaumbele vya timu kuwa ni soka la vijana, kushirikisha wanachama, kutengeneza klabu inayoishi kwenye weledi “Huwezi kushinda kama huna taasisi ambayo ni imara pamoja na kutengeneza mifumo imara, tunaamini kuwa timu inayoongoza Afrika lazima iongeze mapato,”alisema mtendaji huyo. Mwinjuma alisema anaamini klabu hiyo haikuwa na msimu mbaya na inajipanga kwa ajili msimu ujao kufanya vizuri.
“Tunalingaisha, msimu mbaya kwa sababu Simba inashindana na matokeo yake ya nyuma lakini haukuwa mbaya hivyo naamini kwa mipango mlinayo timu kubwa kama Simba haiwezi kuwa na msimu mbaya zaidi ya huu,”alisema Naibu Waziri huyo