Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zirintusa mganda aliyebeba matumaini ya Biashara United

Vnfsgfhg Zirintusa mganda aliyebeba matumaini ya Biashara United

Thu, 15 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Moja ya nyota asiyezungumzwa sana ila amekuwa akifanya mambo makubwa ni Mganda, Boban Zirintusa anayeichezea Biashara United ya mkoani Mara ambaye tangu ajiunge nayo msimu huu akitokea Express FC ya nchini kwao amekuwa na msaada mkubwa.

Nyota huyo aliwahi kuitumikia Mtibwa Sugar ingawa mambo yalikuwa ni magumu kwake na kujitafuta tena upya huku akipita timu mbalimbali kama Polokwane City (Afrika Kusini), Buildcon (Zambia), Ethiopian Coffee (Ethiopia) na Mohun Bagan AC ya India.

Huenda huu ndio msimu bora kwake hapa nchini kwani hadi sasa akiwa na kikosi hicho kinachoshiriki Ligi ya Championship tayari amefunga jumla ya mabao 14 akizidiwa moja tu na kinara, Edgar William wa KenGold anayeongoza na 15.

Mabao hayo ni sawa na yaliyofungwa na kikosi kizima cha Pan Africans ambacho kimefunga 14 katika michezo yake yote 21, iliyocheza hadi sasa huku akiipita Ruvu Shooting inayoburuza mkia kwenye msimamo kwa sababu imefunga jumla ya mabao 10 tu.

Boban hakuanza takribani michezo mitatu ya mwanzo na kikosi hicho tangu msimu huu umeanza ingawa alipoanza kupata nafasi ya kucheza tu tayari amerudisha matumaini mapya ya timu hiyo ya kuamini inaweza kupanda Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao.

Kuonyesha kwa vitendo kwa nyota huyo, kikosi hicho kiko nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi ya Championship kikiwa na pointi 46 nyuma ya vinara KenGold kutoka Mbeya yenye 47 huku kila timu ikiwa imebakisha michezo tisa tu kumalizia msimu.

Umuhimu wa nyota huyo ni mkubwa kwani namba zake zinaongea zaidi kwa sababu katika mabao 36 ambayo timu hiyo imeyafunga yeye ana 14 akiwa na wastani mzuri wa kufunga akishirikiana na Herbert Lukindo ambaye hadi sasa amefunga manane pekee.

KINARA WA ‘HAT-TRICK’

Katika Ligi ya Championship, tayari michezo ya mzunguko wa 21 imeshachezwa na hadi sasa zimefungwa ‘hat-trick’ tano na kati ya hizo Boban amefunga mbili na kuonyesha ni mchezaji aliyebeba matumaini makubwa ya kikosi hicho kwa msimu huu. Nyota huyo alianza kwa kufunga mabao matatu ‘hat-trick’ dhidi ya Ruvu Shooting wakati timu hiyo iliposhinda 3-0, Novemba 11, mwaka jana huku nyingine ya pili akiifunga pia mbele ya Pan Africans katika ushindi wa 4-0, Desemba 11, mwaka jana.

Wengine waliofunga ni Kika Salum wa Pan Africans wakati timu hiyo iliposhinda 3-2, dhidi ya Copco FC Septemba 9, mwaka jana na Abdulaziz Shahame wa TMA FC aliyefunga katika ushindi mnono wa mabao 6-1 na Stand United, Januari 6, mwaka huu.

Nyota wa Mbeya Kwanza, Oscar Mwajanga naye aliingia katika vitabu vya wachezaji waliofunga ‘hat-trick’ na akiwa na kikosi hicho kwenye mchezo wao dhidi ya Ruvu Shooting kilishinda kwa mabao 4-1, mechi iliyopigwa Februari 4, mwaka huu.

Takwimu hizo zinaonyesha wazi nyota huyo amebeba matumaini makubwa ndani ya kikosi hicho kinachohitaji kurudi tena Ligi Kuu Bara baada ya kushuka daraja moja kwa moja msimu wa 2021/2022 kutokana na kukusanya jumla ya pointi 28 katika michezo 30.

MSIKIE MWENYEWE

Akizungumza na Mwanaspoti, Boban anasema siri kubwa ya kiwango chake msimu huu ni kutokana na ushirikiano uliopo kutoka kwa wachezaji wenzake na benchi la ufundi, kwani malengo yao makubwa ni kuirudisha timu hiyo Ligi Kuu Bara msimu ujao.

“Tunacheza kama timu ndio maana tumefikia hapa tulipo, bila wao nisingeweza kufanya hiki ambacho mnakiona kwangu hivyo, ni suala la ushirikiano zaidi na isitoshe bado tuna kazi kubwa ya kufanya mbeleni ili tufikie tunapopahitaji,” anasema.

Kwa upande wa kocha mkuu wa kikosi hicho, Amani Josiah anasema, sababu kubwa ya mchezaji huyo kufanya vizuri ni nidhamu na ushirikiano aliokuwa nao uwanjani na wachezaji wenzake jambo linalomfanya aendelee kuonyesha ubora wake hadi kufikia sasa.

Chanzo: Mwanaspoti