Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zimamoto Moro yataka timu Ligi Kuu

Zimamotooooo Zimamoto Moro yataka timu Ligi Kuu

Sun, 9 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Shaaban Marugujo amesema yuko katika harakati za kusajili timu ya jeshi hilo itakayoshiriki mashindano mbalimbali hapa nchini ikiwa ni pamoja na kucheza Ligi Kuu kama ilivyo kwa timu za taasisi nyingine hapa nchini.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kamanda Marugujo amesema hadi sasa timu hiyo imeshaanzishwa na inacheza michezo mbalimbali ya kirafiki.

“Tumeamua kuanzisha timu ya soka itakayojulikana kama Zimamoto FC na makao makuu yatakuwa hapa Morogoro na tutaitumia hii timu kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana wa hapa Morogoro pamoja na kucheza ligi,” amesema kamanda huyo na kuongeza;

“Kwa kuanzia timu hii itacheza kuanzia ligi za awali na baadaye ndoto zetu ni kuona timu ishiriki Ligi Kuu Bara kama ilivyo kwa timu za taasisi nyingine, kama mmekuwa mkifuatilia taasisi zote zina timu isipokuwa Zimamoto ndio tulikuwa hatuna timu.”

Zoezi la uzinduzi wa timu ya Zimamoto, uliambatana sambamba na mchezo wa kirafiki dhidi ya Choma Nyama na timu hiyo ya jeshi (Zimamoto) kukubali kichapo cha mabao 3-1 mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Ujenzi uliopo Manispaa ya Morogoro.

Kwa upande wa nahodha wa timu hiyo, Benjamini Bandula amesema ujio wa timu hiyo utasaidia ukuaji na uendelezaji wa vipaji kwa vijana.

“Uwepo wa timu hii ya Zimamoto Morogoro utasaidia sisi vijana kupata ajira maana asili ya mkoa huu kuna vipaji vingi vya soka hivyo naamini tutasajiliwa kwa wingi na itakuwa fahari kwetu kuchezea timu ya Zimamoto,” amesema nahodha huyo.

Kwa mujibu wa taratibu za Baraza la Michezo Tanzania (BMT) ili timu iweze kushiriki ligi na mashindano mbalimbali hapa nchini lazima isajiliwe chini ya baraza hilo, lakini lazima iwe na katiba yake, mambo ambayo yanafanyiwa kazi na jeshi hilo.

Chanzo: Mwanaspoti