Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zilipo Simba, Yanga marefa hawa wapo!

Hvduv D Zilipo Simba, Yanga marefa hawa wapo!

Sun, 24 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi Kuu Bara imesimama kupisha kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) na baadhi ya klabu zimeenda mapumziko huku nyingine zikiendelea kujifua kwa ajili ya maandalizi ya mechi zijazo.

Simba na Yanga zipo kambini zikijiandaa na mechi za robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika na Yanga itacheza na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini huku Simba ikipambana na Al Ahly kutoka Misri.

Timu hizo mbili ndio wawakilishi wa Tanzania kwenye mashindano hayo kwa msimu huu, pia ndizo timu zianazofuatiliwa zaidi kwenye Ligi Kuu.

Hadi sasa Yanga ndio kinara wa ligi ikiwa na alama 52 ilizovuna kwenye mechi 20, ikifuatiwa na Azam iliyo nafasi ya pili na pointi 47 baada ya mechi 21 huku Simba ikikaa nafasi ya tatu na alama 45 ilichuma katika mechi 19.

Simba na Yanga kwa jumla zimecheza mechi 39, kwenye ligi hadi sasa, lakini kumbukumbu zilizopo katika mechi hizo zimechezeshwa na marefa wa kati 20 pekee katika mitanange yao na Mwanaspoti hapa linakuletea orodha ya waamuzi waliochezea mara nyingi timu hizo kwa msimu huu hadi sasa.

ARAJIGA

Anaitwa Ahmed Arajiga kutoka Manyara, huyu ndiye mwamuzi aliyechezesha mechi nyingi zaidi zinazohusu Simba au Yanga msimu huu akifanya hivyo mara sita.

Arajiga pia ni kinara kwa kuchezesha mechi za Yanga kwani amefanya hivyo mara nne wakati Yanga ikishinda zote dhidi ya JKT Tanzania 5-0, Azam 3-2, Simba 5-1 na Prisons 2-1.

Aidha Arajiga amechezesha mechi mbili za Simba ikiwemo ile ilipochapwa 5-1 na Yanga sambamba na iliposhinda 3-0 mbele ya Coastal Union.

MWINCHUI

Nassoro Mwinchui ndiye mwamuzi aliyechezesha mechi nyingi za Simba msimu huu hadi sasa. Mwamuzi huyu kutoka Pwani amechezesha mechi tatu za Mnyama akianza na ile iliyoshinda 4-2 dhidi ya Mtibwa, akafuata na ile ya 1-0 dhidi ya Mashujaa kisha ile ambayo Simba ilifungwa 2-1 na Prisons. Mwinchui Hajachezesha mechi ya Yanga msimu huu kwenye ligi.

MROPE

Sady Mrope amechezesha mechi tatu za Yanga msimu huu akianza kwenye ile iliyoshinda 2-0, dhidi ya Singida ikafuata 4-1, na Mtibwa Sugar kisha 2-1 na Mashujaa. Hadi sasa hajachezesha mechi ya Simba msimu huu.

MNYUPE

Anaitwa Ally Mnyupe amechezesha mechi mbili za Yanga akianza na ile Wananchi walipomchapa Tabora 1-0, kisha ile ya 5-0, kwa Ihefu.

Mnyupe pia aliichezesha Simba mechi moja wakati ikiinyuka Tabora United 4-0.

MABENA

Hans Mabena msimu huu amechezesha mechi mbili zinazozihusu Simba na Yanga. Alichezesha mechi moja ya Yanga ilipofungwa 2-1 na Ihefu pia akachezesha mechi moja ya Simba ilipoichapa Kagera Sugar 3-0.

MDOE

Omary Mdoe naye ameingia kwenye historia ya kuchezesha mechi kubwa kwenye ligi kuu. Mdoe amechezesha mechi mbili zote za Yanga dhidi ya KMC akianza na ile ya mabao 5-0, kisha ile ya 3-0. Bado hajachezesha mechi ya Simba hadi sasa.

ESTER

Mwanadada Ester Adelbert naye msimu huu amechezesha mechi mbili zinazozihusu timu vigogo kwenye ligi Kuu.

Ester aliichezesha mechi ya Yanga dhidi ya Dodoma Jiji iliyomalizika mwa Wananchi kushinda 1-0, sambamba na ile ya Simba dhidi ya Tanzania Prisons na Wenye nchi kushinda 3-1.

SASII

Heri Sasii hadi sasa amezichezesha timu zote, Simba na Yanga na alisimamia mchezo wakati Yanga ikichapwa 2-1 na Azam na kukaa kati wakati Simba ikibanwa mbavu na Namungo katika sare ya mabao 1-1.

TATU

Tatu Malogo naye yumo, amechezesha mechi mbili za Simba akianza na ile iliposhinda 2-1, mbele ya Singida Fountain Gate na ile Simba ilipoichapa bao 1-0, JKT Tanzania. Bado hajachezesha mechi ya Yanga msimu huu.

MWANDEMBWA

Emmanuel Mwandembwa ni miongoni mwa waamuzi waliosimamia mechi za timu kubwa nchini na alichezesha mechi za Yanga mbili dhidi ya Namungo 1-0, na Coastal 1-0. Bado hajachezesha mechi yeyote ya Simba msimu huu.

ALLY SIMBA

Anaitwa Ally Simba naye msimu huu amepuliza kipenga wakati timu kubwa ikicheza na aliichezesha Yanga mechi mbili, akianza na ile ya suluhu 0-0 dhidi ya Kagera Sugar kisha ile ya ushindi wa 3-1 mbele ya Namungo. Bado hajachezesha mechi inayoihusu Simba msimu huu kwenye ligi.

MWINYIMKUU

Abdallah Mwinyimkuu alichezesha mechi moja ya Yanga ilipoichapa 3-0 Geita. Bado hajachezesha mechi na Simba msimu huu.

IKAMBI

Raphael Ikambi aliichezesha Yanga mechi moja wakati ikiikanda 1-0 Geita Gold. Hajachezesha mechi na Simba kwenye ligi msimu huu.

MLINA

Gilbert Mlina alichezesha mechi moja ya Simba iliposhinda 2-0 mbele ya Dodoma Jiji. Bado hajachezesha mechi ya Yanga msimu huu kwenye ligi.

AHMADA SIMBA

Ahmada Simba aliingia kwenye vitabu vya kuchezesha timu kubwa msimu huu alipoichezesha Simba ikishinda 2-1 mbele ya Ihefu. Bado hajachezesha mechi ya Yanga hadi sasa kwa msimu huu.

MANIABA

Thabit Maniaba yumo pia kwani alichezesha mechi moja ya Simba ilipotoa sare ya mabao 2-2 na KMC. Bado hajaichezesha Yanga msimu huu.

KAYOKO

Ramadhan Kayoko alichezesha mechi moja ya Simba dhidi ya Azam iliyomalizika kwa sare ya mabao 1-1. Bado hajachezesha mechi iliyohusu Yanga kwenye ligi msimu huu.

RUKYA

Jonesia Rukya msimu huu amechezesha mechi kubwa moja ya Simba na Mnyama ilishinda 1-0, mbele ya Geita Gold.

HUSSEIN

Hussein Athuman naye alichezesha mechi moja kubwa ambayo Simba ilishinda 2-1, mbele ya Coastal. Bado hajachezesha mechi ya Yanga msimu huu.

KATANGA

Katanga Hussein alichezesha mechi moja kubwa kati ya Simba na Singida na Simba kushinda kwa mabao 3-1. Bado hajachezesha mechi ya Yanga msimu huu.

WAJIHI

Mwamuzi Abdi Wajihi amechezesha mechi moja kubwa wakati Simba inashinda 2-1 mbele ya Mashujaa. Msimu huu bado hajachezesha mechi hata moja ya Yanga.

Chanzo: Mwanaspoti