Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zilianza Ligi Kuu kwa kasi, sasa zinaporomoka

42a6ae0c94e8d63f2fc4fa81cddad8c8 Zilianza Ligi Kuu kwa kasi, sasa zinaporomoka

Fri, 16 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

LIGI Kuu soka Tanzania Bara inaendelea na kuonesha ushindani mkubwa kiasi baadhi ya timu zilianza vizuri lakini sasa zinazidi kuporomoka na nyingine zimeshindwa kumudu ushindani, zinateseka.

KMC

Ukiitazama timu ya Manispaa ya Kinondoni (KMC) namna ilivyoanza ligi na inakoelekea, sijui wamepatwa na nini ghafla kwasababu sio wale walioanza kwa kasi ya kuwatisha wengine.

KMC ilianza michezo miwili kwa nguvu na kupata ushindi tena ilikuwa ni timu ambayo iliogopwa, hasa katika michezo ya awali baada ya kufunga mabao mengi kuliko nyingine yoyote.

Mchezo wake wa kwanza walicheza dhidi ya Mbeya City wakaibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0. Ikiwa ndio timu pekee iliyopata ushindi mkubwa katika michezo ya ufunguzi.

Na bado ikaendeleza ubora katika mchezo wa pili wakashinda mabao 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons na dhidi ya Mwadui mabao 2-1 ugenini.

Matokeo hayo yaliifanya KMC kuwa kinara katika uongozi wa Ligi Kuu ikiongoza kwa pointi tisa michezo mitatu ya awali na pia, kwa idadi kubwa ya mabao na wengine wakifuatia.

Timu hiyo ilitajwa kuwa na ubora katika safu ya ushambuliaji na kupata sifa nyingi kupitia usajili wake.

Lakini ni kama wamejiloga baada tu ya kufanya vizuri michezo hiyo na kuanza kupata upinzani mkali tofauti na matarajio.

Kitendo cha kupoteza mchezo wa nne dhidi ya Kagera Sugar bao 1-0, kilianza kuwaporomosha kutoka kwenye uongozi na kumpisha Azam FC aliyekuwa akimkimbiza.

Tangu ipopoteze, bado KMC haijarudi katika kiwango chake na takwimu zinaonesha baada ya kupoteza dhidi ya Polisi Tanzania bao 1-0 na kusuluhu dhidi ya Coastal mchezo wa mzunguko wa sita wanaweza kuzidi kuporomoka ikiwa wengine wanaofuatana watashinda.

Timu hiyo bila shaka inapaswa kujitathmini mwenendo wake na kujirekebisha kabla mambo hayajazidi kuwa magumu zaidi na kujiingiza katika presha za kupigania matokeo mazuri baadaye.

Licha ya hayo yote, bado KMC wana kikosi kizuri chenye ushindani na wakijipanga vizuri watarudi katika kasi yao walioanza nayo.

IHEFU FC

Timu hii bila shaka imeshindwa kumudu ushindani wa ligi na kadiri siku zinavyokwenda mambo yanazidi kuwa magumu kwao.

Nani anaweza kuamini kiwango walichokionesha dhidi ya Simba watakuja kushuka namna hii? Walicheza soka la kiushindani kuonesha namna gani wamejipanga na kumbe ilikuwa nguvu ya soda.

Ihefu ni miongoni mwa timu zilizopanda daraja msimu huu na baada ya kufungwa kwa tabu na bingwa mtetezi wa ligi Simba mabao 2-1 katika mchezo wa ufunguzi, walitabiriwa kuleta ushindani.

Kasi waliyoanza nayo awali iliwapa nafasi ya kujiamini na kufanya vizuri mchezo wa pili dhidi ya Ruvu Shooting baada ya kushinda bao 1-0.

Huo ulikuwa ni ushindi wa kwanza na wa mwisho na sasa mambo yanazidi kuwa mabaya baada ya kupoteza dhidi ya Mtibwa bao 1-0, dhidi ya Mwadui mabao 2-0, dhidi ya Gwambina mabao 2-0 na dhidi ya Biashara United.

Takwimu hizo zinaonesha ni mjanja anapokuwa nyumbani, lakini katika viwanja vya ugenini ameshindwa kabisa kuondoka na pointi yoyote.

Bila shaka hapaswi kutegemea matokeo ya nyumbani ni lazima ajipange na ugenini kupata matokeo hata kama sio ya ushindi angalu sare ili kumwezesha kuwa sehemu nzuri.

Huenda akirejea katika uwanja wake wa nyumbani atarudi katika kiwango na kasi aliyoanza nayo awali.

JKT TANZANIA

JKT Tanzania ni moja ya timu ambazo zimekuwa zikileta ushindani tangu msimu uliopita.

Katika mchezo wao wa kwanza wa ligi walianza vizuri kwa kufunga ugenini bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar.

Mchezo huo ulitabiriwa huenda wakaendeleza kasi yao kama ilivyokuwa huko nyuma, lakini ukiitizama namna wanavyosogea mbele ndivyo ambavyo wanazidi kuporomoka.

Timu hii inaonekana kushindwa kumudu ushindani wa ligi katika mechi za awali baada ya kuwa na mwenendo mbaya.

Ilichapwa dhidi ya Dodoma Jiji mabao 2-0, dhidi ya Coastal bao 1-0, dhidi ya Simba mabao 4-0 na dhidi ya Ruvu bao 1-0 ikatoka sare mchezo mmoja wa bao 1-1 dhidi ya Polisi Tanzania.

Wanahitaji kubadilika na kujitathmini ni wapi wanakosea na kujipanga upya kabla mambo hayajazidi kuwa mabaya huko mbele. Nafasi wanayo na kuna mechi nyingi mbele wanaweza kubadilisha matokeo.

KAGERA SUGAR

Mwenendo wa timu hii ukilinganisha na msimu uliopita sio mzuri. Timu hii inaporomoka kwasababu haina matokeo mazuri.

Imetoka kupoteza dhidi ya Namungo mabao 2-1, dhidi ya Azam FC mabao 4-2, dhidi ya Yanga bao 1-0 na dhidi ya JKT Tanzania. Imeshinda mchezo mmoja dhidi ya KMC na kupata sare moja dhidi ya Gwambina 0-0.

Matokeo hayo ni dalili kuwa wanashindwa kumudu ushindani na wapo hatarini zaidi kuendelea kuporomoa kama hawatabadilisha matokeo yao kuwa mazuri.

Hizi ni baadhi tu zipo nyingi zinapishana kutoka nafasi za juu kurudi chini na nyingine zinapanda juu.

Zilizoko hatarini na zinazoweza kuingia kwenye mkumbo huo ni Coastal Union, Tanzania Prisons, Mtibwa na Mwadui. Itategemea na mechi zao zilivyokwenda au zitakavyokuwa.

Siku zinavyozidi kwenda, Ligi Kuu Tanzania Bara inazidi kuwa ngumu, hivyo timu lazima zifuate usemi wa `biashara asubuhi na jioni ni kazi ya kuhesabu mapato tu’. Kazi kwenu.

Chanzo: habarileo.co.tz