Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zile shoo za Mapinduzi Cup zinaanza sasa

Simba Zanzibar Mapinduzi.jpeg Zile shoo za Mapinduzi Cup zinaanza sasa

Mon, 1 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 ilianza tangu Alhamisi iliyopita kwa kupigwa mechi sita tofauti (hii ni kabla ya mbili za jana za Kundi C), lakini mashabiki wa soka visiwani Zanzibar wanasema sasa ndo shoo za maana zimeanza wakati Simba itakapotupa karata ya kwanza kwa msimu huu kuikabili JKU.

JKU huo ni mchezo wa pili kwao baada ya awali kufumuliwa mabao 4-1 na Singida Fountain Gate ambayo mapema saa 10:15 jioni) itavaana na APR ya Rwanda kabla ya Simba na JKU kuumana kuanzia saa 2:15 usiku, mechi zote zikipigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, mjini Unguja.

Mechi hizo zinapigwa ikiwa ni siku ya kwanza ya Mwaka Mpya wa 2024 na Simba iliyoingia visiwani humo mchana wa jana, itashuka uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya msimu uliopita ilipovaana na Mlandege na kujikuta ikilala bao 1-0 lililochangia kuing’oa mapema.

Kwa upande wa JKU ambao ni vinara wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), ikijua kupoteza mchezo huo huenda ikajiweka kwenye hatari ya kuaga michuano hiyo inayochezwa kwa msimu wa 18 tangu ilipoasisiwa kwa mfumo wa sasa mwaka 2007.Simba iliyo chini ya Kocha Abdelhak Benchikha imeingia Zenji na mziki wote ukiondoa wachezaji waliopo timu za taifa zinazojiandaa na Fainali za Afcon, akiwamo Clatous Chama ambaye hata hivyo alisimamishwa kwa muda usiojulikana na uongozi kwa utovu wa nidhamu sambamba na Nassor Kapama.

Kipa namba moja kwa sasa, Ayoub Lakred ni kati ya nyota wapya wa timu hiyo ambao wapo visiwani kwa ajili ya pambano hilo la kwanza akiwamo Fabrice Ngoma, Willy Onana, Luis Miquissone, Fondoh Che Malone, Abdallah Khamis, Hussein Kazi na wengine ambao wana dhima ya kuibeba timu hiyo Mapinduzi.

Hata hivyo, kikosi cfha Simba kinapaswa kuwa makini na JKU kwani ni wazi timu hiyo itashuka uwanjani ikiwa na kiu ya kutaka kusahihisha makosa ili isipoteze mchezo wa pili unaoweza kuwang’oa michuanoni.

Huu utakuwa mchezo wa tatu kwa timu hizo kukutana kwenye michuano hiyo, baada ya awali kukutana 2015 na 2016 na mara zote Simba kuibuka mbabe, kitu kinachoipa kazi JKU kutaka kulipa kisasi mbele ya Mnyama.

Mapema kocha wa Simba, Benchikha alisema ataitumia michuano hiyo kuwaangalia wachezaji wasiopata nafasi kikosini ili kufanya maamuzi wakati dirisha dogo likiwa wazi, huku taarifa kutoka kambini zinasema kocha huyo amewataka wachezaji kupambana ili kuwapa raha mashabiki na kurejea na taji hilo.

Simba ndio klabu iliyocheza fainali nyingi ya Mapinduzi ikifanya hivyo mara nane na kutwaa mataji manne ikiwa ni klabu ya pili nyuma ya Azam yenye mataji matano katika fainali sita ilizocheza tangu ilipoanza kushiriki michuano hiyo ilipopanda Ligi Kuu msimu wa 2008-2009.

Bila shaka mashabiki wa soka watapata burudani kwenye Uwanja wa Amaan, lakini kabla ya pambano hilo mapema nyasi za uwanja huo zitawaka moto wakati Singida itakapokuwa ikisaka ushindi wa pili wa kuivusha kwenda robo fainali itakapoikabili APR.

Kocha wa Singida, Thabo Senong alikiri kundi hilo ni gumu kutokana na aina ya timu walizopangwa nazo huku akiweka wazi hiyo haiondoi wao kuendelea kuwa bora kwenye kila mchezo.

“Kundi B tulilopo ni gumu sana, tuna timu nyingi zenye ubora na uzoefu mkubwa mfano leo tunakutana na APR timu ambayo licha ya kuwa ni mara yao ya kwanza kushiriki mashindano haya lakini ni timu bora,” alisema Senong na kuongeza;

“Tunacheza na timu ambayo ina kikosi bora na uzoefu mkubwa wa mashindano tumejiandaa kupambania malengo yetu ya kuhakikisha tunacheza fainali na hatimaye kutwaa taji.”

Nahodha wa Singida, Gadiel Michael alisema wanaingia kwenye mchezo huo kwa kuwaheshimu wapinzani huku akikiri leo wanacheza mchezo wa kimataifa dhidi ya timu bora.

“Matokeo tuliyoyapata kwenye mchezo uliopita tumeyasahau licha ya kutuongezea morari sasa kisaikolojia tumejiandaa kushindana na APR bira kuangalia tulichokipata nyuma tunahitaji kufika fainali na hatimaye kutwaa taji,” alisema.

Kocha wa APR, Thierry Froger alisema licha ya ugumu wa ratiba ya michuano hiyo amekiandaa kikosi chake kuhakikisha kinapata matokeo mazuri dhidi ya Singida leo.

“Ni michuano ambayo ina ratiba ngumu mchezo mmoja mapumziko siku moja hii inatupa wakati mgumu kama makocha kuandaa kikosi vizuri lakini nafurahi nimekuja na kikosi kipana nitatumia vizuri mashindano haya kujiandaa kwaajili ya kujiweka fiti kwa mzunguko wa pili wa ligi nchini Rwanda,” alisema Froger, huku kiungo wa zamani wa Simba ambaye sasa anakipiga APR, Sharaf Shiboub alisema sio mgeni kwenye michuano hiyo licha ya kushiriki akiwa kwenye timu ngeni wamejiandaa vizuri kushindana.

“Tumejiandaa vizuri na timu ipo kwenye morali nzuri, tuna nafasi ya kupambana na kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hii,” alisema .

Chanzo: Mwanaspoti