Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zijue ndoa nne za Marc Anthony, kuachana na Jennifer Lopez

Marc Anthony Na Jennifer Lopez Marc Anthony na Jennifer Lopez

Mon, 20 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwimbaji maarufu duniani, Marc Anthony bado hapoi wala haboi linapokuja suala la ndoa, Jumamosi iliyopita huko Miami, Florida alifunga ndoa yake ya nne ndani ya miaka 23 na Miss Universe Paraguay, Nadia Ferreira.

Haikuweza kufahamika mara moja ikiwa mapacha wake, Emme na Max, 15, ambao wanaishi na aliyekuwa mkewe, Jennifer Lopez kama walihudhuria, pamoja na watoto wake wawili aliyopata aliyekuwa mpenzi wake, Debbie Rosado, Arianna, 29, na Chase, 27,.

Anthony, 54, na Ferreira, 23, walijumuika na marafiki mbalimbali mashuhuri, akiwemo David Beckham na mkewe, Victoria Beckham, Salma Hayek, Lin Manuel Miranda, Luis Fonsi, Romeo Santos na Maluma.

Wawili hao waliibua tetesi kuwa ni wapenzi kufuatia matembezi yao huko Mexico City na walithibitisha uhusiano wao kupitia Instagram kwa kuposti picha ya ‘selfie’ iliyopigwa kwenye ndege binafsi Machi mwaka jana.

“Mungu na uzidishe yote unayotutakia.” aliandika katika chapisho lake Instagram mwimbaji huyo wa kubao maarufu, I Need to Know.

Walitangaza kuchumbiana kwao Mei 2022 wakati wa sherehe katika Mgahawa wa Sexy Fish huko Miami, Florida, huku Ferreira akionyesha picha ya pete yake kubwa ya almasi aliyovishwa na Anthony kwenye Insta Story yake.

Kwa ujumla Marc Anthony amefunga nne kama ifuatavyo na kujaliwa kupata watoto wanne ingawa kwa ujumla ana watoto sita ambapo wawili aliwapata kati ya mwaka 1994 na 1995 kabla ya kufunga ndoa yoyote.

Antony & Dayanara Torres (2000 – 2004) Anthony alifunga ndoa na aliyekuwa Miss Universe 1993, Dayanara Torres kutokea Mexico Mei 9, 2000, huko Las Vegas, Marekani na kujaliwa watoto wawili, Cristian Marcus Muniz aliyezaliwa Februari 5, 2001 na Ryan Adrian Muniz aliyezaliwa Agosti 16, 2003.

Kulikuwa na matatizo mengi katika ndoa yao hadi kupelekea kutengana mwaka 2002 ila baadaye walipatanishwa na kufanya upya viapo vyao vya ndoa katika sherehe rasmi iliyofanyika Desemba 7, 2002, katika Kanisa Kuu la San Juan huko Puerto Rico.

Hata hivyo, ndoa hiyo ilikuja kuvunjika Oktoba 2003 huku Dayanara akiomba talaka Januari 2004, ili kumsaidia kupona maumivu kutokana na talaka hiyo, Dayanara alibadilisha pete yake ya ndoa na saa aina ya Cartier iliyopambwa na almasi, huku akiandika kitabu chake, Married to Me: How Committing to Myself Led to Triumph After Divorce.

Anthony & Jennifer Lopez (2004 – 2014) Hadi sasa hii ndio ndoa pekee ya Marc Anthony iliyodumu kwa muda mrefu zaidi, miaka 10, Anthony alimuoa Jennifer Lopez (J.Lo) Juni 5, 2004 na walikuwa wamefanya kazi pamoja hapo awali na inaripotiwa kuwa uhusiano wao ilianza mwishoni mwa miaka ya 1990.

Walishirikiana kwenye muziki kwa kutumbuiza pamoja na kuigiza katika filamu, El Cantante (2006), kufika Februari 22, 2008 J.Lo alijifungua watoto wao mapacha, Emme Maribel Muniz na Maximilian David Muniz.

Baada ya mafanikio katika ndoa na biashara, Aprili 9, 2012 Anthony na J.Lo walitangaza kutengana, Anthony aliwasilisha kesi ya talaka yao iliyokamilishwa Juni 16, 2014, huku Lopez akihifadhi haki ya msingi ya kuwalea watoto hao wawili.

Anthony & Shannon De Lima (2014 – 2017) Hii ndio ndoa ya Marc Anthony iliyodumu kwa muda mfupi zaidi, miaka mitatu, Anthony na Mwanamitindo Shannon De Lima kutokea nchini Venezuela walifunga ndoa Novemba 11, 2014, huko La Romana, Jamhuri ya Dominika.

Ikumbukwe kabla ya kuolewa na Anthony, De Lima tayari alikuwa na uhusiano na Alejandro Sosa na kujaliwa kupata mtoto wa kiume, Daniel aliyezaliwa Oktoba 29, 2007, na sasa yupo na mcheza soka, James Rodriguez.

Novemba 2016, Anthony na De Lima walitengana na mwezi uliofuata wakatangaza kuwa wanashughulikia talaka, Februari 13, 2017, Anthony na De Lima walikamilisha talaka yao, huku wakiwa hajafanikiwa kupata mtoto katika kipindi cha miaka mitatu ya ndoa.

Anthony & Nadia Ferreira (2023) Tangu mwaka 2000 hadi 2017 katika ndoa zake tatu, kila mwaka ambao Marc Anthony angeachana na mwanamke, basi mwaka huo huo angefunga ndoa nyingine, lakini tangu alipoachana na Shannon De Lima mwaka 2017 alijipa likizo ya ndoa kwa miaka mitano.

Anthony na Ferreira walifunga ndoa Januari 28, 2023 kwenye Jumba la Makumbusho la Perez huko Florida ikiwa ni takribani mwaka mmoja tangu kuanza uhusiano wao.

Ikumbukwe Nadia Ferreira aliyezaliwa Mei 10, 1999 alitawazwa kuwa Miss Universe Paraguay 21 na alipowakilisha nchi hiyo katika mashindano ya urembo ya Miss Universe 2021 alishika nafasi ya pili, pia aliwahi kuwa mshindi wa tatu wa Miss Teen Miss Universe Paraguay 2015.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live