Gwiji wa Real Madrid na Ufaransa, Zinedine Zidane amemwambia Lionel Messi kwamba alitamani kucheza na gwiji huyo wa Barcelona katika wakati fulani wa maisha yake ya soka.
Katika zama zake za kucheza soka, Zidane alikabiliana na Messi mara moja tu mwaka 2005, katika mechi ambayo Mfaransa huyo timu yake ya Madrid ililala 3-0 katika La Liga dhidi ya Barcelona, huku Muargentina huyo akitoa asisti ya bao mojawapo siku hiyo. Hata hivyo, magwiji hao wawili hawakuwahi kucheza katika kikosi kimoja.
Zidane amebainisha kwamba angependa siku moja angebahatika kucheza katika kikosi kimoja na nyota huyo ambaye sasa anaitumikia klabu ya Inter Miami. Katika mazungumzo yao yaliyowezeshwa na adidas, Zidane alisema: "Ni jambo baya kwamba hatukuwahi kucheza pamoja. Angalau muda huu ndio muda ambao nakupasia mpira. Leo ni siku muhimu sana kwangu kwa sababu napata wasaa wa kukwambia vile ambavyo ninakukubali… naamini (wewe) jamaa ni muujiza, muujiza halisi."
Aliposema hivyo, Messi akarudisha sifa hizo, akisema: "Daima nimekuwa nikukubali sana. Nimekufuatilia sana pale Madrid. Na ulinifanya nipate mateso sana kwa sababu mimi nilikuwa natokea Barcelona!"
Kisha wawili hao wakazungumzia mambo mbalimbali. Wakajadili kuhusu hisia walizopata kwa kufungia bao timu zao za taifa katika mechi ya fainali ya Kombe la Dunia. Kisha wakaeleza heshima walizonazo kwa gwiji wa soka wa Argentina, Diego Maradona, na pia wakajadili kuhusu upungufu wa wachezaji Namba 10 katika soka la kisasa duniani.
Messi anashikilia rekodi ya muda wote ya kushinda mara nyingi zaidi tuzo ya Ballon d’Or ya Mwanasoka Bora wa Mwaka akiitwaa mara nane wakati Zidane aliitwaa tuzo hiyo mara tatu na akiwa mchezaji na kocha wa Real Madrid alishinda mataji manne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (Uefa Champions League) na matatu ya Ligi Kuu ya Hispania, La Liga.