Ligi Kuu Zanzibar kwa msimu wa 2023-2024 inafikia tamati jioni ya leo wakati zitakapopigwa mechi saba za kukamilisha raundi ya 30, ambapo bingwa mpya wa ligi hiyo anatarajiwa kufahamika rasmi, huku JKU ikijiweka pazuri mbele ya Zimamoto zikiwa timu pekee zenye nafasi ya kubeba taji.
Awali, ligi hiyo ilitarajiwa kumalizika Juni 17, lakini kutokana na uwepo kwa michuano ya fainali za Kombe la Shirikisho (FA) kwa Unguja na ile ya Taifa ndio maana linamalizika leo baada ya jana KMKM na Mlandege kufunga rasmi msimu zilipovaana, huku Mabaharia wa KMKM waliotema taji la ZPL wakishinda 2-1 na kumaliza katika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 57.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana usiku na Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) ni kwamba mechi za kumalizia msimu zinapigwa leo Ijumaa kisha sherehe za kukabidhi bingwa mpya wa ligi hiyo zitafanyika Jumapili kwa pambano maalumu litakalozikutanisha bingwa huyo wa ZPL na Bingwa wa Ligi Daraja la Kwanza Kanda ya Unguja, Muembe Makumbi.
Taarifa hiyo imesema mgeni rasmi wa sherehe hizo anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Tabia Maulid Mwita na shughuli zitaanza mara baada ya mchezo huo utakaopigwa kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, mjini Unguja.
Mechi zitakazopigwa leo ni pamoja na ile ya mapema saa 7:30 mchana kati ya mabingwa wa Kombe la Shirikisho, Chipukizi itakayoialika Uhamiaji kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba kabla ya saa 10:30 jioni kupigwa nyingine sita za kufunga msimu huu.
Kati ya michezo hiyo sita, ule ya New City dhidi ya Zimamoto unatupiwa macho kama ulivyo wa Kipanga itakayovaana na JKU kutokana na ukweli ndizo zilizoshikilia hatma ya ubingwa kwa msimu huu baada ya KMKM iliyokuwa ikilishikilia taji hilo kwa misimu mitatu mfululizo kulitema mapema.
JKU ndio inayoongoza msimamo kwa muda mrefu ikiwa na pointi 65, ikihitaji moja tu mbele ya Kipanga ili kufikisha 66 ambazo haziwezi kufikiwa na Zimamoto yenye alama 62 inayohitaji ushindi mbele ya New City na kuiombea JKU ipoteze kwa Kipanga na kubeba ubingwa kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa. JKU ina mabao 44 na kufungwa 22 wakati Zimamoto imefunga mabao 51 na kufungwa 21.
New City inapambana kuepuka kushuka daraja ikiwa ina pointi 34 na bado haipo salama iwapo timu zilizopo nyuma za Kundemba na Hard Rock zitashinda mechi zao zitaivuta hadi nafasi ya 13 na kuungana na Maendeleo, Jamhuri na Ngome zilizoshuka mapema kabla ligi haijafikia tamati.
Mechi ya New City na Zimamoto itapigwa kwenye Uwanja wa Mao B, huku ya JKU na Kipanga itachezwa kwenye Uwanja wa Amaan B
Mechi nyingine ni kati ya Jamhuri v KVZ (Uwanja wa FFU Finya, Pemba), Malindi v Kundemba (Mao A), Mafunzo v Ngome (Amaan A) na ile ya Maendeleo na Hard Rock itapigwa Gombani.
Timu za Kundemba yenye pointi 32, Hard Rock (33) na New City (34) zenyewe zitakuwa uwanjani huku zikiombeana mabaya ili kujinusuru kushuka daraja kuzifuata timu tatu zilizotangulia, kwani kwa mujibu wa kanuni timu nne za mwisho zinashuka daraja moja kwa moja.