Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zawadi za tuzo za mwezi Ligi Kuu mh!

Maxi Mpia Nzengeli Kiungo wa Yanga, Maxi Mpia Nzengeli

Mon, 22 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Tuko mwaka 2024 na Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2023/24, inakaribia kuingia mzunguko wa pili.

Cha ajabu ni kwamba hadi muda wa kuandika makala hii, wasimamizi wa mashindano yaani bodi ya ligi hawajatoa zawadi hata mara moja ya mwezi kwa washindi wa tuzo za mwezi.

Hii ni ajabu sana. Tunakaribia Februari ya mwaka 2024, zawadi za washindi wa tuzo za kuanzia Agosti ulipoanza msimu, hawajapata zawadi zao.

Washindi wenyewe

Agosti

Kocha bora: Gamondi -Yanga

Mchezaji bora: Maxi Nzengeli – Yanga

Septemba

Kocha bora: Abdihamid Moallin - KMC

Mchezaji bora: Waziri Junior – KMC

Oktoba

Kocha bora: Robertinho - Simba

Mchezaji bora: Azi Ki – Yanga

Novemba

Kocha bora: Bruno Ferry - Azam FC

Mchezaji bora: Feisal Salum - Azam FC

Desemba

Kocha bora: Bruno Ferry - Azam FC

Mchezaji bora: Kipre Jr. - Azam FC

Tuzo hizi ambazo husimamiwa na kamati ya tuzo ya TFF, hudhaminiwa na wadhamini wa ligi kuu, Benki ya NBC na Azam TV.

Ni aibu kwa TFF na wadhamini hawa kushindwa kutoa zawadi kwa washindi hadi sasa, miezi takribani sita tangu kuanza kwa msimu.

Swali ni kwamba, je wadhamini wamefulia kiasi cha kushindwa kutoa zawadi au wametoa halafu wasimamizi yaani TFF wamekula?

Hii inakuja wakati Watanzania bado wapo kwenye mjadala wa pesa za zawadi kwa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 15.

Mwezi Desemba mwaka jana iliibuka taarifa ya TFF kuchikichia zawadi ya shilingi milioni 188 ya timu ya taifa chini ya miaka 15, waliyopata baada ya kushika nafasi ya pili kwenye mashindano ya CECAFA.

Taarifa hii iliyoanza kama tetesi kupitia mitandao ya jamii, ilikuja kuthitibishwa Rais wa TFF, Wallace Karia, akasema kwamba fedha hizo zitatumika kujengea miundombinu.

Rais Karia alitoa ufafanuzi huo baada ya presha kubwa sana kutoka kila kona ya nchi kufuatia baadhi ya wachezaji kufichua siri.

Bila hivyo TFF isingesema chochote.

TFF ninayoizungumzia hapa ndiyo hii ambayo haijatoa zawadi kwa washindi wa tuzo za mwezi.

Isijekuwa kumbe fedha zao zimetumika vinginevyo?

ZAWADI ZENYEWE

Kwa kuwa msimu huu bado hakuna mshindi aliyepewa zawadi yake, tutumie zawazi za msinu uliopita kama ushahidi wa kiasi kinachotolewa.

Washindi wa mwisho msimu uliopita walikuwa Saido Ntabanzonkiza kama mchezaji na Robertinho kama kocha, waote kutoka Simba.

Kwa ushindi huo, kila mmoja alipata shilingi milioni moja za Tanzania, pamoja na kisimbuzi cha Azam TV.

Ukipiga hesabu hapa kwa kwa fedha taslimu utapata shilingi milioni 10. Na ukihesabu visimbuzi pia utapata 10.

Siyo ajabu TFF ikawa imechukua visimbuzi hivi na kuvifunga kwenye hosteli zao za Kigamboni na Tanga na kwenye ofisi zao.

Sisemi kwamba wamefanya hivyo, bali najaribu kuunganisha nukta kutokea kwenye zawadi za wale vijana wa chini ya miaka 15.

Waswahili wanasema kimya kingi kina mshindo mzito. TFF inapokaa kimya kuhusu hizo tuzo, inasababisha kishindo kikubwa na kuleta hofu kwa watu.

Na nyinyi wadhamini, benki ya NBC na Azam TV, jitokezeni mseme kitu la sivyo watu watawaunganisha na huu ukimya mchafue sifa yenu.

Hakuna majibu yoyote yanayoweza kueleweka hapa, zaidi ya kutoa zawadi.

Kamati ya tuzo kupitia hili inazidi kujivua nguo kuthibitisha ni kiasi gani haiyawezi majukumu yake.

Tuzo zenyewe mara kadhaa zimekuwa zikitolewa kwa upendeleo na kuacha maswali mengi.

Ukiacha tuzo za mwezi, tuzo za mwaka ndiyo kizunguzungu.

Washindi wengine husababisha watu wanaoangalia tuzo waone aibu kama wao ndiyo walichagua.

Msimu uliopita, walimpa Clement Mzize wa Yanga tuzo ya mchezaji bora wa U20.

Hii ilikuwa ajabu sana kwa sababu Mzize hakushiriki ligi ya vijana chini ya miaka 20 msimu uliopita, yeye alishiriki msimu wa nyuma yake.

Mchezaji bora wa U20 msimu uliopita alikuwa Ladack Chasambi wa Mtibwa Sugar na alitangazwa baada ya mashindano pale Chamazi.

Sasa kamati yenye madudu kama haya inapokutana na TFF yenye madudu yale ya juu halafu kwa pamoja wakachelewesha zawadi, inaleta mashaka kwamba yawezekana kuna kitu wamekitengeneza juu kwa juu.

Chonde chonde kamati ya tuzo, chonde chonde TFF. Toeni zawadi za washindi wa ligi kuu wa tuzo za kila mwezi.

Chanzo: Mwanaspoti