Timu za Simba na Yanga zipo kwenye michuano ya kimataifa kwa msimu huu na hadi sasa zinaonekana kuwa zina nafasi kubwa ya kufuzu kwa hatua ya robo fainali ya michuano hiyo, lakini majina waliyopeleka Caf yakinaswa.
Simba tayari wana pointi tatu kati michezo mitatu ya Kombe la Klabu Bingwa na Yanga wana pointi nne katika michezo mitatu ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kanuni za mashindano ya CAF pamoja na mambo mengine zinazitaka timu zote zinazoshiriki kwenye michuano hiyo mikubwa kuwasilisha umri wa wachezaji wao kwenye Shirikisho la Soka la Tanzania TFF na baadaye Caf ikiwa ni moja jambo muhimu sana ambalo linatakiwa.
Mashabiki wa soka wamekuwa wakilalamika mara kwa mara kwua baadhi ya wachezaji wa timu za Simba na Yanga umri wao unawatupa mkono, lakini data hizi ambazo Mwanaspoti limezipata zinaonyesha jambo la tofauti.
Taarifa ya umri ambayo ipo TFF na Caf inaonyesha kuwa wachezaji wengi wa timu hizo hawana umri mkubwa kama ambavyo inaelezwa na mashabiki wengi wa timu hiyo ingawa kumekuwa na mawazo tofauti kwa mashabiki wengine wakiamini kuwa wamedanganya na wengine wakiamini kuwa wapo sahihi.
Hata hivyo, kocha wa timu ya Dodoma Jiji, Merlis Medo, amesema kama mchezaji anadanganya umri ni sawa na kujindangaya mwenyewe kwa kuwa makocha wengi wamekuwa wakigawa mazoezi kutokana na umri wa wachezaji.
"Dunia nzima mchezaji akidanganya umri anakuwa amejidanganya mwenyewe, mchezaji mwenye umri mdogo anaweza kufanya mazoezi kwa dakika 120 kwa kutumia nguvu kidogo sana, lakini mchezaji mwenye umri mkubwa atakuwa anashindwa kufanya mazoezi hayo hayo kwa dakika 45, haijalishi kocha utamsukuma kwa kiwango gani lakini akishindwa ameshindwa hata umfanye nini," alisema Medo.
Makocha mbalimbali wamekuwa wakizigawa timu zao kwenye madaraja matatu tofauti kwenye umri wa wachezaji ambao wanaamini kuwa ndiyo wanaweza kuwa na balansi nzuri, inaonekana kuwa timu bora inatakiwa kuwa na wachezaji wachache wenye umri chini ya miaka 23, wengi wenye umri wa miaka 23 hadi 28 na wachache tena wenye umri wa miaka 28 hadi 35.
Timu nyingi zimekuwa zikitengeneza vikosi vyao bora kwa kutumia umri wa wachezaji na mara nyingi timu zenye wachezaji vijana tupu au wazee tupu zimekuwa zikishindwa kufanya vizuri na inaaminika kuwa ile yenye wachezaji wazee imekuwa na kasi mwanzoni mwa msimu na kushindwa kumaliza vizuri hasa kama ligi husika ina michezo mingi.
Lakini kwenye ile yenye wachezaji wengi vijana imekuwa ikionyesha kiwango kizuri uwanjani na kuwa na wakati mgumu wa kupata matokeo.
YANGA
Kikosi cha Yanga kwa mujibu wa takwimu zilizopelekwa Caf kinaonyesha kuwa mchezaji wao kijana kuliko wote kati ya majina yao ni Clement Mzize ambaye anaonekana akiwa amezaliwa mwaka 2004, akiwa na umri wa miaka 18 akiwa amepandishwa na Yanga kutoka kwenye kikosi cha vijana, Denis Nkane anafuata akiwa anaonekana kuwa amezaliwa mwaka 2002, ikiwa inaonyesha kuwa ana umri wa miaka 20 sasa.
Wengine wanaofuata ni wachezaji watatu wa Yanga ambao wamezaliwa mwaka 2020 ambao ni Shomari Kibwana, Dickson Job na Yusuf Athumani, kati yao wawili wakiwa wana nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza mara kwa mara na Athumani akiwa kwa mkopo kwenye kikosi cha Coastal Union kinachoshriki Ligi Kuu Tanzania.
Hata hivyo, listi hiyo inaonyesha kuwa mchezaji mwenye umri mkubwa kuliko wote kwenye kikosi cha Yanga ni Zawadi Mauya ambaye ana umri wa miaka 35, baada ya kuzaliwa mwaka 1988, akiwa anafuatiwa na Salum Abubakar aliyezaliwa mwaka 1992, akafuata ni Khalid Aucho aliyezaliwa mwaka 1993, sawa na Joyce Lomalisa halafu Yanick Bangala ambaye amezaliwa mwaka 1994.
Kikosi cha Yanga kinaonekana kuwa na balansi nzuri ya wachezaji wenye umri mzuri wa kati kikiwa na wachezaji nane wenye umri wa miaka 20-27, umri ambao wataalamu wa soka wanasema kuwa ndiyo kipindi kizuri zaidi kwa wachezaji kutumika kwenye timu, chini ya miaka 20 Yanga inaonekana ina mchezaji mmoja tu na juu ya miaka 30 ina wachezaji saba.
Majina baadhi ya Yanga yaliyotumwa Caf na umri wao:
Metacha Manata (25.11.1998) 25
Ibrahim Hamad (12.11.1997) 26
Bakari Mwamnyeto (05.11.1997) 26
Yanick Bangala (12.04.1994) 29
Dickosn Job (29.12.2000) 23
Feisal Salum (11.01.1998) 25
Lazalous Kambole (20.01.1994) 29
Khalid Aucho (08.08.1993) 30
Fiston Mayele (24.06.1994) 29
Stephan Aziz Ki (06.03.1996) 27
Jesus Moloko (02.06.1997) 26
Lomalisa Joyce (18.06.1993) 30
Yusuph Athuman (28.02.2000) 23
Kibwana Shomari (01.01.2000) 23
Denis Nkane (30.09.2002) 21
Farid Mussa (21.06.1996) 27
Salum Abubakar (26.08.1992) 31
Zawadi Mauya (26.11.1988) 35
Djuma Shaban (16.03.1993) 30
Brayson Daud (06.11.1998) 25
Abdallah Shaibu (21.10.1998) 25
Kennedy Musonda (22.12.1994) 29
Mamadou Doumbia (28.02.1995) 28
Mudathir Yahya (06.05.1996) 27
Abutwalib Mshery (02.02.1999) 24
Tuisila Kisinda (20.05.1993) 30
Erick Johola (12.06.2000) 23
Bernard Morrison (20.05.1993) 30
Gael Bigirimana (22.01.1993) 30
Dickson Ambundo (09.03.1996) 27
Djigui Diarra (27.02.1995) 28
Clement Mzize (07.01.2004) 19.
SIMBA
Kwa upande wa Simba, hakuonekana kuwa na tofauti kubwa na Yanga ambapo wachezaji wengi wanaonekana kuwa kwenye wastani mzuri wa umri tofauti na maneno ambayo yamekuwa yakisemwa mtaani.
Kwa mujibu wa listi iliyotumwa Caf, inaonyesha kuwa wachezaji wengi wa Simba ni wa miaka ya tisini na wachache sana wamezaliwa nyuma ya hapo, mchezaji mdogo zaidi kwa Simba ni Ahmed Feruz akiwa amezaliwa mwaka 2002 akiwa na umri wa miaka 21, lakini akiwa ni mchezaji ambaye hapati nafasi sana na mchezaji ambaye anapata nafasi kwenye timu hiyo ni Jean Baleke mwenye miaka 22, akiwa amezaliwa mwaka 2021, anafuatiwa na Ahmed Musa ambaye naye ana miaka 22 wakiwa wanafuata Habib Kyombo, Kibu Denis na Peter Banda.
Hata hivyo, tofauti na matarajio ya wengi, Simba ambayo ipo kwenye nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu, anayeongoza kwa kuwa na umri mkubwa ni Saido Ntibazonkiza akiwa amezaliwa mwaka 1987 kwa sasa, akiwa na umri wa miaka 36 anafuatiwa na Erasto Nyoni ambaye ana umri wa miaka 35, Joash Onyango amezaliwa mwaka 1993, akiwa sasa ana umri wa miaka 30.
Kwa wastani Simba wanaonekana hawana mchezaji hata mmoja aliye chini ya miaka 20, lakini wakiwa na wachezaji tisa ambao wana umri wa kuanzia miaka 20 hadi 25, wachezaji 12 wana umri wa kuanzia miaka 25 hadi 30 na wachezaji sita wenye miaka 30 na kuendelea.
Baadhi ya wachezaji wa Simba na umri wao
Aishi Manula (13.09.1995) 28
Hamed Sawadogo (28.02.1996) 27
Pape Sakho (21.12.1996) 27
Shomari Kapombe (28.01.1992) 31
Mohamed Hussein (01.11.1996) 27
Joash Onyango (31.01.1993) 30
Clatous Chama (18.08.1991) 32
Mzamiru Yasin (03.01.1996) 27
John Bocco (05.08.1989) 34
Henock Inonga (25.11.1994) 29
Said Ntibazonkiza (01.05.1987) 36
Jean Baleke (17.04.2001) 22
Israel Mwenda (10.03.2000) 23
Jonas Mkude (03.12.1992) 31
Moses Phiri (03.06.1994) 29
Kennedy Juma (07.08.1994) 29
Benno Kakolanya (27.06.1994) 29
Habibu Kyombo (21.12.2000) 23
Mohamed Ouattara (28.06.1999) 24
Kibu Denis (04.12.2000) 23
Peter Banda (21.12.2000) 23
Erasto Nyoni (07.05.1988) 35
Gadiel Michale (12.09.1996) 27
Sadio Kanoute (21.10.1996) 27
Mohamed Musa (22.09.2001) 22
Jimson Mwanuke (14.01.1999) 24
Augustine Okrah (22.09.1993) 30
Ahmed Feruzi (20.02.2002) 21
Nassoro Kapama (15.12.1996) 27
MAKOCHA WANENA
Kocha wa Ihefu Zuber Katwila amesema mara nyingi umri unategemea kocha anataka nini.
"Inategemea kocha ama nchi husika inataka nini, mfano Italia wana wachezaji wa umri mkubwa wanaotoka klabu nyingine, Ufaransa wachezaji wao ni wa umri mdogo na Uingereza ni mchanganyiko.
Aliongeza :"Unaweza ukawa na wa umri mdogo wasikupe matokeo kama wakubwa, lakini faida ya umri mdogo wanakuwa na nguvu zaidi ila wanakosa uzoefu, hivyo mchanganyiko kwenye kikosi inategemeana na kocha anauchanganya vipi.
"Kocha akijua mchezaji mkubwa hawezi kumuacha akafanya mazoezi dakika zote na wale chipukizi lazima kuna muda atamtoa, pia kwa wiki lazima atampuzisha mkongwe kwani anakuwa anajua umri sahihi wa wachezaji wake, ila nasisitiza wanatumika wote kutokana na kile wanachokifanya uwanjani."